Ofisi Ya Jengo La Utawala Halmashauri Ya Wilaya Ya Busega Yakabidhiwa


Ofisi ya Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Busega limekabidhiwa tayari kwa matumizi. Makabidhiano hayo yamefanyika siku ya Jumatatu tarehe 9 Novemba, 2020. Jengo la Utawala limekabidhiwa na Mkandarasi wa Ujenzi wa Jengo hilo Kampuni ya BMB kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya  Busega Anderson Njiginya, pia tukio hilo limeshuhudiwa na Mhandisi Mshauri kampuni ya NEDCo na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega.

Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Busega lina jumla ya vyumba 97 ambapo jumla ya vyumba 68 vikiwa tayari kwa matumizi, ambayo ni zaidi ya asimilia 70% ya ukamilikaji wa jengo lote. Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Busega lilianza kujengwa mnamo Mwaka 2015 ambapo Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliweka Jiwe la Msingi Mwaka 2016.

Aidha Jengo hilo ambalo likikamilika lote litagharimu jumla ya TZS Bilioni 4.9 linatatua changamoto ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kukosa miundombinu na mazingira bora ya kufanyia kazi, kwani jengo linalotumika kwa sasa halikidhi idadi ya watumishi. Aidha kukabidhiwa kwa jengo hilo kunapunguza gharama ya fedha zilizokuwa zikitumika kwaajili ya kulipia jengo linalotumika kwasasa tangu hapo Halmashauri ilipoanzishwa mwaka 2013.

MWISHO.





from MPEKUZI

Comments