Rais Magufuli aomboleza vifo vya raia 15 Kagera Waliofariki Kwa Ajali


Rais Dkt. Magufuli ameeleza kupokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya watu 15 vilivyosababishwa na ajali ya barabarani baada ya basi la abiria kupinduka katika mteremko wa Kumnyange uliopo katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.

Katika salamu zake za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brig. Jen Marco Gaguti, Dkt. Magufuli amemtaka afikishe salamu za pole kwa familia za marehemu, ndugu, jamaa na wote walioguswa na vifo hivyo, na amewaombea Marehemu wote wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka na kuungana na familia zao.

“Nimesikitishwa na vifo vya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, nawapa pole wafiwa wote na nawaomba wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi kigumu cha majozi,” amesema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wa barabara hasa madereva wa magari kuzingatia sheria zote za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Pia amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani kuchukua hatua dhidi ya watumiaji barabara wanaokiuka sheria za barabarani.

Ajali hiyo ambayo imetokea leo tarehe 24 Oktoba, 2020 pia imesababisha watu 18 kujeruhiwa.


 


from MPEKUZI

Comments