Wanafunzi Shule ya Msingi Wachomana Visu

Mwanafunzi funzi wa darasa la saba Shule ya Msingi Azimio Wilaya ya Tarime mkoani Mara mwenye miaka 15, anatafutwa na polisi kwa tuhuma za kumchoma kisu na kumuua mwanafunzi mwenzake, Rhobi Chacha (14).

Kamanda wa polisi Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema tukio hilo lilitokea juzi na Rhobi alifariki dunia saa sita mchana wakati akipata matibabu Hospitali ya Mji wa Tarime.

Marehemu alikuwa mwanafunzi wa darasa la tano Shule ya Msingi Azimio na mkazi wa Iganana, kata ya Sabasaba, Tarime.

“Baada ya kitendo hicho mtuhumiwa alikimbia na polisi tunamtafuta ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Mwaibambe.

Kaimu mganga mkuu wa Hospitali ya Mji Tarime, Dk Innocent Kweka alisema alimpokea Rhobi juzi saa nne asubuhi lakini alifariki dunia akiendelea na matibabu.

“Kwenye uchunguzi ilibainika kuwa alichomwa na kitu chenye incha kali na kilizama kwenye mapafu, hali iliyosababisha marehemu kuvuja damu na kupoteza maisha,” alisema Dk Kweka.

Akizungumzia tukio hilo mwalimu mkuu msaidizi shuleni hapo, Bahati Lucas alisema Rhobi na Charles wanasoma shuleni hapo. “Inasikitisha sana, mtuhumiwa alikuwa anatarajia kufanya mtihani wake wa mwisho wa darasa la saba mwaka huu,” alisema.

Naye mwenyekiti wa mtaa wa Iganana, Edward Thomas alisema mtuhumiwa na Rhobi ni majirani wanaotenganishwa na barabara ya mtaa. 

“Ulizuka ugomvi kati yao wakati wanacheza mpira, mtuhumiwa aliingia nyumbani na kuchukua kisu na kumshambulia mwenzake,” alisema Thomas.



from MPEKUZI

Comments