Umoja wa Ulaya (EU) kutoa Bilioni 780 kwa wakimbizi na Watanzania Kigoma

Umoja wa Ulaya (EU) wameahidi kutoa msaada wa Sh780 bilioni kwa wakimbizi waliopo mkoani Kigoma na wananchi pembezoni mwa kambi ya wakimbizi hao.

Ahadi hiyo imetolewa leo Juni 30, 2018 na balozi wa Ujerumani nchini,  Dk Detlef Wachter alipotembelea kambi ya Nduta iliyopo Kibondo mkoani Kigoma akiwa na mabalozi wengine kutoka nchi za EU.

Wakimbizi wamepangiwa kupata Sh390bilioni huku Watanzania wakipangiwa Sh390bilioni kwa ajili ya kuboresha huduma za kijamii na kuwawezesha wananchi kiuchumi ili waondokane na umasikini.

Amesema msaada huo utaongeza uhusiano kati ya wakimbizi na wananchi wanaoishi jirani na kambi.

Balozi wa EU, Roeland Van de Geer amesema kwa miaka mingi Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR) walikuwa wanasaidia wakimbizi, sasa mkakati umebadilika na wameanza kusaidia jamii ya wenyeji.

Kaimu Mkuu wa Wilaya Kibondo, Dk Gabriel Chitupila ameishukuru EU kwa misaada wanayotoa huku akisisitiza wasaidie kuboresha huduma za kijamii kama afya, elimu, maji na hifadhi ya mazingira.

Mkoa wa Kigoma una kambi tatu za wakimbizi ambazo ni Nyarugusu, Nduta na Mtendeli zenye zaidi ya wakimbizi 350,000 kutoka Burundi na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC).


from MPEKUZI

Comments