Ujerumani OUT kombe la dunia nchini Urusi

Timu ya taifa ya Ujerumani imevuliwa rasmi ubingwa wa Kombe la Dunia baada ya kukubali kichapo cha bao 2-0 kutoka kwa Korea Kusini.

Ujerumani ambayo kabla ya kuanza kwa fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia, ilikuwa ikipigiwa chapuo la kutetea ubingwa wake lakini leo iliingia uwanjani ikiwa na matarajio ya kupata ushindi kirahisi.

Hata hivyo mambo yakawa tofauti na matarajio yao, katika mchezo huo uliopigwa Kazan Arena, mjini Kazan kiasi kwamba kadiri muda ulivyokwenda Ujerumani walikutana na kizingiti kutokana na mfumo uliotumiwa na Kocha wa Korea Kusini, Shin Tae-yong wa 4-4-2 ambao ulikuwa wa kujilinda zaidi.

Hilo liliwafanya kupoteza umakini na kupiga mipira mingi isiyo na malengo jambo lililosababisha timu hizo kwenda mapumziko zikiwa hazifungana.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Ujerumani walijaribu kusaka bao la kuongoza lakini kukosa umakini kwa washambuliaji wake kukawa kiwazo.

Kocha wa Ujerumani, Joachim Löw aliyetumia mfumo wa 4-2-3-1 na benchi lake la ufundi walikua katika wakati mgumu sana ilipofika dakika ya 60 huku matokeo yakiendelea kuwa bila bila wakati matokeo ya mechi nyingine ya kundi hilo yakionyesha kuwa Sweden ilikua ikiongoza kwa mabao 2-0 dhidi ya waliokua vinara wa kundi hilo kabla ya mechi hizo Mexico.

Kitendo cha Mesut Ozil kushindwa kuuweka mpira wavuni katika dakika ya 62 kuliwakera Low na hata mashabiki wa Ujerumani ambao walianza kuona dalili za kuvuliwa ubingwa wao katika raundi ya kwanza.

Ujerumani walianza kuvuliwa ubingwa baada ya Kim Young-Gwon kufunga bao la kwanza katika dakika ya pili ya muda wa nyongeza, jambo lililowafanya wachezaji wote kupagawa na kipa wa Ujerumani Manuel Neuer aliamua kulicha lango lake na kwenda mbele kusaidia kusaka bao.

Uamuzi huo ukawa kama kaa la moto kwao kwani mpira mrefu ulionaswa na Son Heung-Min ulimfanya mshambuliaji huyo wa Korea Kusini kulikimbilia lango lililokuwa tupu na hivyo kufunga bao rahisi katika dakika ya mwisho ya muda wa nyongeza.

Kuingia kwa bao hilo kuliangusha kilio kwa wachezaji, viongozi  na mashabiki wa Ujerumani ambao tayari walifahamu fika kuwa wamevuliwa ubingwa katika raundi ya kwanza kwani tayari Sweden walikua wameilaza Mexico mabao 3-0 kuashiria kuwa ndio waliokua vinara wa kundi F na Mexico wanashika nafasi ya pili zote zikiwa na pointi sita, Korea Kusini wamemaliza wa tatu na Ujerumani wameburuza mkia kwenye kundi hilo wakiwa na pointi tatu.


from MPEKUZI

Comments