TCRA yavipiga faini vituo vya redio kwa kukiuka kanuni

Kamati ya maudhui ya mamlaka ya mawasiliano (TCRA) imevitoza faini ya Sh6 milioni vituo vya redio vya Magic Fm na Rasi Fm kwa kukiuka kanuni za maudhui.

Akisoma hukumu hiyo Juni 29, 2018 Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Joseph Mapunda amesema Magic Fm cha Dar es Salaam, imetozwa faini ya Sh4 milioni kwa kosa la kukiuka kanuni za utangazaji kwa kushindwa kuweka mizania wakati wakichambua bajeti ya wizara ya mifugo.

Kupitia kipindi chake cha ‘Morning Magic’ kilichorushwa Mei 18 mwaka huu mtangazaji alieleza kuhusu kufilisika kwa kampuni ya uvuvi ya Taifa (Tafico) na kampuni ya ranchi za taifa (Narco).

Kwa mujibu wa kamati hiyo, watangazaji walitoa taarifa bila kupata maoni ya upande wa serikali na vilevile hawakuwa na uhakika wa taarifa walizozitoa.

Kwa upande wa Rasi Fm cha Dodoma, kilikutwa na hatia ya kukiuka kanuni za utangazaji kwa kurusha maudhui ya ngono katika muda ambao wasikilizaji wake wengi ni watoto.

Mapunda amesema Juni 6 mwaka huu saa tano asubuhi mtangazaji alizungumzia kuhusu ngono na uangaliaji wa filamu za ngono jambo linalowahamasisha vijana na watoto kuwa na tabia mbaya.

Kutokana na hilo kituo hiki kimekutwa na makosa mawili ikiwamo kushindwa kuwalinda watoto na kuweka mada za wakubwa muda ambao wasikilizaji ni watoto.

Kila kosa lilitozwa faini ya Sh1 milioni zinazotakiwa kulipwa ndani ya siku 30 kuanzia leo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Rasi Fm Ramadhan Mkotsollah amesema ameridhishwa na uamuzi huo kwa kuwa kweli kosa lilifanyika.

"Ni kweli kulingana na taratibu hilo ni kosa na mie binafsi sikufurahishwa na kitendo hicho ndio sababu tumechukua hatua,"amesema


from MPEKUZI

Comments