WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali katika ngazi zote wawajibike ipasavyo kwenye ukusanyaji wa mapato na kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha na rasilimali za Taifa.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itaimarisha ukaguzi katika ngazi zote na ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo na kufanya tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha kwamba miradi na kazi zitakazofanyika zinawiana na thamani ya fedha (Value for money) za umma zinazotolewa na Serikali.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) katika hotuba yake aliyoitoa bungeni wakati wa kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge jijini Dodoma.
Vilevile, Waziri Mkuu amesema taasisi zote za Serikali zinasisitizwa kutumia mifumo ya kieletroniki kukusanya mapato na wafanyabiashara wote wanahimizwa kutumia mashine za EFD na kulipa kodi kwa hiari.
Amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba malengo ya ukusanyaji wa mapato na matumizi yanazingatia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. “Viongozi na watendaji wote wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za matumizi ya fedha za umma katika eneo la ukusanyaji wa mapato,”.
Waziri Mkuu amesema Serikali itasimamia ipasavyo utekelezaji wa bajeti sambamba na kuongeza uwajibikaji na nidhamu ya matumizi ya fedha zilizoelekezwa katika vipaumbele mbalimbali kama ilivyoidhinishwa na Bunge.
Amesema katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali itashirikiana na sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi wote kwa ujumla ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika mwaka 2018/2019, Serikali imepanga kutumia jumla ya sh. trilioni 32.48. Kati ya fedha hizo, sh. trilioni 20.47 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya Bajeti na sh. trilioni 12.01, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wadau wa kilimo, mifugo, uvuvi na sekta nyingine watumie fursa mbalimbali zinazopatikana katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDPII),ili kutimiza ndoto ya Taifa kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
Aidha, Waziri Mkuu ameziagiza taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa ASDP II, ziimarishe usimamizi na ufuatiliaji ili utekelezaji wa mpango huo uwe na mafanikio makubwa.
Amesema mpango huo unaweka mkazo katika maeneo makuu manne, ambayo ni usimamizi endelevu wa matumizi ya ardhi na maji katika kilimo; kuongeza tija na faida katika kilimo, mifugo na uvuvi; kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza thamani ya mazao na kuwajengea uwezo wadau wa sekta katika uratibu, ufuatiliaji na tathmini.
Juni 4, 2018, Rais Dkt. John Magufuli alizindua Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini (ASDP II), ikiwa na lengo la kuongeza tija na uzalishaji katika mnyororo wote wa thamani ili kuvipatia malighafi viwanda vitakavyoanzishwa na kupata ziada ya kuuza katika masoko ya nje ya nchi na kupata faida kubwa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment