Muhogo Sasa Rasmi Kwenye Mazao Ya Biashara.....Ni baada ya kupata soko kubwa nchini China

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya China imetoa fursa ya kufungua soko la muhogo mkavu kutoka Tanzania, tukio ambalo  linafungua ukurasa mpya wa zao la muhogo kuwa miongoni mwa mazao ya biashara.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) bungeni jijini Dodomakatika hotuba yake aliyoitoa wakati wakuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge.

Amesema ili kuwezesha wakulima na wafanyabiashara wa Tanzania kunufaika na fursa hiyo, Mei, 2018 ulisainiwa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya China kuruhusu bidhaa za muhogo mkavu kutoka Tanzania kuingia katika soko la China. 

Amesema kufuatia hatua hiyo, mwezi huu wa Juni 2018, tani 74 za muhogo mkavu kutoka Tanzania zimeingia China kupitia Bandari ya Qingdao iliyopo katika jimbo la Shandong.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema kiasi cha muhogo kilichofanikiwa kuingizwa katika soko la China bado ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji ambayo yanazidi tani 150,000 kwa mwaka.

Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania wachangamkie fursa ya kilimo cha muhogo ambacho kimeonesha kuwa na tija kubwa, pia amevitaka vituo vya utafiti wa kilimo viwawezeshe wakulima kupata mbegu bora na mbinu za kisasa ili waongeze uzalishaji na kukidhi mahitaji ya soko hilo.

Waziri Mkuu amesema kutokana na zao la muhogo kuonekana kuwa na matumizi menginezaidi ya chakula, Serikali inaendelea kuvutia uwekezaji wa viwanda vya kuchakata muhogo na kuzalisha bidhaa mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwamba umekuwa na mafanikio katika maeneo mengi nchini kwa sababu wakulima wadogo na wa kati wapo kwenye ushirika, hivyo kuwa na nguvu ya soko na bei nzuri ya mazao yao.

“Mathalani, kwa kutumia mfumo huo, mwezi huu bei ya ufuta imeongezeka kutoka shilingi1,500 hadi shilingi 2,800 kwa kilo na kuua mfumo usio rasmi wa uuzaji wa zao hilo ujulikanao kama ‘chomachoma’ ambao  ulimpunja mkulima kwa ujazo na bei,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amesema mfumo huo unasaidia kuzuia upotevu wa mazao unaotokana na uhifadhi dhaifu, pia unasaidia kuhifadhi mazao ili kusubiri kuuza wakati muafaka na kuyaongezea thamani mazao kabla ya kuyauza.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa mfumo huo unatekelezwa kikamilifu na kuleta tija kwa wakulima.

Amesema hatua hizo ni pamoja na ushirikishwaji wa wadau, kuimarisha ushirika, kuweka miundombinu ya masoko na kuboresha muundo wa taasisi na vitendeakazi vya Bodi ya Stakabadhi za Ghala.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watendaji Serikalini kuhakikisha kuwa mazao mengi zaidi yanaingizwa katika stakabadhi za ghala ili kuwe na tija kwa wakulima.


from MPEKUZI

Comments