Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala (RCO) Atoa Ushahidi Kesi ya Halima Mdee Dhidi ya Rais Magufuli

Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala (RCO), Davis Msangi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa alibaini maneno yaliyotamkwa na mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ni ya jinai wakati akiangalia mtandao wa kijamii wa you tube kupitia simu yake.

Msangi ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka aliyaeleza hayo jana Ijumaa Juni 29, 2018 wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kutoa lugha ya matusi inayomkabili Mdee.

Katika kesi hiyo Mdee anadaiwa kuwa alifanya kosa hilo Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema yaliyopo mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni.

Anadaiwa kumtukana Rais John Magufuli kuwa “anaongea ovyo ovyo, anatakiwa afungwe breki” kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Halima alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Julai 10, 2017.

Akiongozwa na wakili wa Serikali, Patrick Mwita kutoa ushahidi, Msangi amedai kuwa Aprili 2017 hadi Januari 2018 alikuwa mkuu wa upelelezi wilaya ya Kinondoni.

Shahidi huyo wa kwanza wa upande wa mashtaka amedai kuwa Julai 4, 2017 alikuwa ofisini kwake na kupitia simu yake katika mtandao wa you tube aliona kichwa cha taarifa iliyoandikwa Magufuli afungwe breki.

Msangi amedai aliifungua na kuisikiliza maudhui ya ndani na kwamba yeye kama mlinzi wa amani aliona kuna jinai, kwamba alimuona Mdee akizungumza maneno hayo na alifuatilia na kutambua kuwa alikuwa katika mkutano na waandishi wa habari.

Alibainisha kuwa maudhui yalikuwa ni maneno kuongewa kwa sauti na kwamba kilichomfanya aone kuna jinai ni maneno yaliyoongelewa kuwa rais ana mambo ya ovyo ovyo anatakiwa afungwe breki.

Amebainisha kuwa baada ya kupata kipande cha video ya Mdee katika mkutano huo kutoka kwa Abdul, akatambua kuwa alichokiona you tube hakikuwa cha kutengeneza, hivyo kufungua jalada la uchunguzi.

Alidai kuwa baada ya kuipata video hiyo, aliituma kwa mtaalam wa matukio kutoka maabara ya kisayansi polisi makao makuu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 11, 2018 siku ambayo mashahidi wa upande wa mashtaka wataendelea kutoa ushahidi katika kesi hiyo.


from MPEKUZI

Comments