SERIKALI imesema Mwekezaji wa kampuni ya Asas Dairies Ltd ameahidi kufunga mitambo ya kuchakata maziwa kama kiasi cha maziwa kitaongezeka kwenye wilaya ya Busokelo.
Aidha, kwa sasa mwekezaji anakusanya jumla ya lita 3600 za maziwa kwa siku.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Busokelo(CCM) Fredy Mwakibete.
Mwakibete katika swali lake, alihoji serikali ina mpango gani wa kusaidia kumalizia kiwanda cha maziwa kinachojengwa kata ya Isange hasa ikizingatiwa maziwa mengi yanaharibika kwa kukosa soko.
Alisema Busokelo ni miongoni mwa Halmashauri zinazozalisha maziwa ya ng’ombe kwa wingi ambayo kwa mwaka inazalisha zaidi ya lita milioni 50.
Akijibu swali hilo, Ulega alisema kiwanda hicho kilianza kujengwa na serikali mnamo mwaka 2012 chini ya program ya kuendeleza sekta ya kilimo ya awamu ya kwanza.
“Kupitia program hiyo Sh.Milioni 140 zilitolewa na kutumika kujenga jengo la kiwanda, kuingiza umeme, maji na ununuzi wa tenki la kupoza maziwa lenye ujazo wa lita 2030,”alisema.
Aidha alisema uibuaji wa ujenzi wa kiwanda cha Maziwa cha Isange ulitokana na ukosefu wa soko la maziwa na hivyo kufanya maziwa mengi kuharibika.
Hata hivyo alisema ujenzi wa kiwanda ilikwama baada ya kumalizika kwa Programu ya kuendeleza sekta ya Kilimo awamu ya kwanza(ASDP I) ambayo ilikuwa ikifadhili Mradi wa kiwanda hicho.
“Halmashauri ya wilaya ya Busokelo ilitangaza fursa ya uwepo wa jengo la kiwanda cha maziwa kwa ajili ya wawekezaji ambapo mwekezaji wa Asas Dairies Ltd alijitokeza na kuomba kuwekeza katika jengo la kiwanda cha maziwa,”alisema.
Kadhalika, alisema Mwekezaji baada ya kuingia mkataba na Halmashauri ameanza kutumia jengo hilo kama Kituo kikubwa cha kukusanyia maziwa yanayonunuliwa kutoka kwa wafugaji kupitia ushirika wa wafugaji wa maziwa na Utambuzi na sasa mwekezaji anakusanya jumla ya lita 3600 za maziwa kwa siku.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment