Watumishi Wa Umma Waaswa Kuwa Kioo Katika Kuzingatia Maadili


Na. James K. Mwanamyoto-Monduli

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaasa watumishi wa umma kuwa na maadili ili kujenga taswira nzuri ya Serikali kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zitolewazo na taasisi za umma nchini. 

Mhe. Ndejembi ametoa wito huo kwa watumishi wa umma nchini, wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, akiwa katika ziara ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamozo zinazowakabili watumishi wa umma katika Wilaya hiyo ya Monduli.

Mhe. Ndejembi amesema watumishi wa umma ndio kioo cha jamii, na ni taswira ya Serikali katika jamii, hivyo wanapaswa kuwa na maadili mema yatakayolinda haiba ya Serikali na utumishi wa umma kwa ujumla.

“Mtumishi wa umma hapaswi kuwa mlevi wa kupindukia au kuwa na tabia ambazo hazipendezi katika jamii inayokuzunguka, kwani tabia hizo zinaharibu taswira nzuri ya utumishi wa umma,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.

Aidha, Mhe. Ndejembi amewataka watumishi wa umma kuzingatia utunzaji wa siri za Serikali wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, ili taarifa na nyaraka za Serikali ziendelee kuwa katika mikono salama ya Serikali yenyewe.

“Watumishi wa umma hakikisheni mnatunza siri zote za Serikali mnazozifahamu kupitia utendaji kazi wa shughuli zenu za kila siku, ili kuviishi viapo vyenu mlipoajiriwa,” Mhe. Ndejembi amehimiza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Mhe. Frank Mwaisumbe amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kuhimiza uadilifu kwa watumishi wa wilaya yake, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kiutumishi.

Naye, Afisa Maendeleo ya Jamii, Bi. Rose Mhina kwa niaba ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, amemshukuru Mhe. Ndejembi kwa kusikiliza kero na changamoto zinawakabili na kuzifanyia kazi papo kwa hapo, ikiwa ni pamoja na kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali za kiutumishi walizoziwasilisha. 

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo.



from MPEKUZI

Comments