Tamko La Serikali Kuhusu Tishio La Mgomo Wa Madereva


Ndugu Wanahabari; Kama mnavyokumbuka mnamo tarehe 22 Julai, 2022 Serikali ilitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kushughulikia Hoja na Malalamiko yaliyowasilishwa na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji nchini.

Kufuatia kutolewa kwa taarifa hiyo, wapo baadhi ya Madereva ambao wameipokea kwa mtazamo tofauti.

Kutokana na hali hiyo, wamekuwa wakipotosha taarifa hiyo na kuchochea ama kuhamasisha Madereva wenzao kugoma.

Uchochezi wa mgomo wao umejikita katika viwango vya posho ambavyo Madereva, Wamiliki wa Vyombo vya Usafiri na Serikeli waliafikiana katika vikao vya majadiliano.

Ndugu Wanahabari; Viwango walivyokubaliana ni viwango vya chini vya posho za
safari (Minimum allowances) ambapo waajiri hawaruhusiwi kulipa chini ya viwango
hivyo.

Kwa wale Waajiri ambao walikuwa wanalipa viwango ambavyo viko juu ya viwango vya chini vya posho za safari vilivyowekwa, hawaruhusiwi kushusha viwango hivyo kwani kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa Sheria.

Ndugu Wanahabari; Serikali kwa kutambua umuhimu wa sekta ya usafirishaji kwa uchumi wa nchi, inasisitiza kuwa nafasi ya majadiliano bado ipo wazi na hivyo Wafanyakazi Madereva ambao wana hoja na malalamiko zaidi ya yale yaliyofanyiwa kazi, wayawasilishe rasmi katika mamlaka zinazohusika ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.

Ndugu Wanahabari; Ninawasihi Wafanyakazi Madereva wapokee kwa mtazamo chanya
taarifa ya Serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kushughulikia Hoja na Malalamiko yaliyowasilishwa na Vyama vyao na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji.

Ninawasihi Wafanyakazi Madereva wote kuendelea kutekeleza majukumu yao kama kawaida. Natoa rai
kwa makundi yanayojihusisha kuchochea migomo ya Madereva kuacha mara moja, kwanikufanya hivyo ni kukiuka Sheria.

Hivyo, Serikali haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wale wote watakaoendelea kuchochea migomo ya Madereva.
IMETOLEWA NA
Prof. Joyce Lazaro Ndalichako (MB)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU
(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

from MPEKUZI

Comments