HESLB: Dirisha La Kuomba Mkopo Kufunguliwa Kabla Ya Julai 15


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema dirisha la uombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 linatarajia kufunguliwa kabla ya tarehe 15 Julai, 2022. 

Katika taarifa yake iliyotolewa  Jumatano Julai 6, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji wa HESLB (pichani), Abdul-Razaq Badru ilisema HESLB inakamilisha taratibu za uombaji mikopo kwa mwaka 2022/2023 na dirisha litafunguliwa katika kipindi cha siku 10 zijazo.

“Taarifa hii inatolewa kufuatia maombi mengi ya taarifa ya ufafanuzi kutoka kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka 2022 na matokeo yao kutangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA),  Jumanne Julai 5, 2022.” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru.

Badru amesema kwa sasa waombaji mikopo watarajiwa wanatakiwa kuwa watulivu na kuanza maandalizi ya awali ya kuandaa nyaraka muhimu kama vyeti vyao vya kuzaliwa au vyeti vya vifo vya wazazi wao vilivyohakikiwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Wakala wa Usajili wa Matukio Muhimu Zanzibar (ZCSRA).

Kuhusu sifa na utaratibu wa kuomba mkopo kwa mwaka 2022/2023, Badru amesema maelezo yatapatikana katika ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa mwaka 2022/2023’ utakaoanza kupatikana katika tovuti ya HESLB https://ift.tt/od2tzTh 15, 2022.

HESLB ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na majukumu ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wanaojiunga na taasisi za elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika.



from MPEKUZI

Comments