Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo sasa ni mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
DRC imeidhinishwa rasmi kuwa mwanachama wa saba wa EAC baada ya Christophe Lutundula, Naibu Waziri Mkuu Anayeshughulikia Masuala ya Nje ya Kongo DR kukabidhi nyaraka kwa makao makuu ya jumuiya hiyo ya kikanda huko Arusha, Tanzania.
Hatua ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuidhinishwa rasmi kuwa mwanachama kamili wa EAC ina maanisha kuwa, nchi hiyo sasa ina haki zote za nchi mwanachama wa jumuiya hiyo, na itafaidi mambo mengi kama wanachama wengine.
Baadhi ya mambo itakayofaidi DRC baada ya kupasishwa rasmi kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuruhusiwa raia wake kuingia katika nchi wanachama wa jumuiya bila viza.
Vile vile soko lake litapanuka kutokana na uagizaji na usafirishaji huru wa bidhaa hususan katika maeneo ya mashariki ya kanda hiyo ya Afrika, yanayotegemea bandari za Mombasa na Dar es Salaam. Aidha nchi hiyo sasa ina haki ya kuteua wanachama 9 wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) na majaji wa Mahakama ya Uadilifu ya jumuiya hiyo EACJ.
Peter Mathuki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema mchakato wa DRC kujiunga na jumuiya hiyo umekamilika, na sasa ni rasmi nchi hiyo ni mwanachama kamili wa EAC.
Sudan Kusini ilikuwa nchi ya mwisho kukubaliwa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Machi mwaka 2016, kabla ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kukubaliwa kujiunga na jumuiya hiyo Machi mwaka huu.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment