Serikali imetaka ushirikiano na wadau wa kupinga utumikishwaji wa kazi kwa watoto ili kufanikiwa kukomesha utumikishwaji huo hapa nchini.
Wadau ambao hawanabudi kutoa ushirikiano madhubuti kwa Serikali ni pamoja na Mashirika ya Kimataifa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Vyama vya Wafanyakazi, Vyama vya Waajri, Asasi za Kidini na za Kiraia pamoja na wananchi.
Hayo ameyasema jijini Dodoma Juni 12, 2022, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Patrobasi Katambi, wakati wa kuadhimisha siku ya Kupinga Utumikishwaji wa kazi kwa watoto Duniani.
Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni:
" Utumikishwaji wa Watoto ni Kikwazo cha Maendeleo Endelevu, Wadau Tushikamane Kuutokomeza"
Mhe. Katambi, amesisitiza kila mdau kuhakikisha haki za msingi za watoto zinalindwa kwa kutimiza wajibu wake.
"Katika kutokomeza Utumikishwaji wa Watoto katika kazi hatarishi lazima mzingatie matakwa ya Mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) na mapendekezo yake kupitia Sheria za Kazi za hapa nchini"
Mhe.Katambi ameongeza kuwa, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Serikali (Integrated Labour Force Survey) wa mwaka 2014, umeonesha, 29% ya watoto wenye umri kati ya miaka 5- 17 sawa na watoto millioni 4.2, wavulana wakiwa ni 29.3% na wasichana 28.4% wako katika utumikishwaji .
Aidha, amefafanua kuwa utafiti huo umebainisha kuwa, watoto wengi wapo katika sekta za kiuchumi ikiwa ni pamoja na mashambani, majumbani, migodini, na biashara ndogondogo.
Kwa mujibu wa utafiti huo, sababu kuu zinazo chochea matukio ya utumikishwaji ni Umasikini, Vifo vya Wazazi na Walezi, Mifarakano katika Familia, Mila na Desturi zisizofaa pamoja na Nguvu Kazi Rahisi (Cheap Labour).
Pia, unabainisha madhara ya moja kwa moja yanayosababishwa na utumikishaji wa watoto ni Kuwa na Taifa la Watu Wasiojua Kusoma na Kuandika pamoja na Kuenea kwa Magonjwa kama vile UKIMWI.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Mtoto ametafsiriwa kuwa ni mtu yeyote mwenye Umri wa chini ya miaka 18.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment