Asila Twaha , OR – TAMISEMI
Serikali imetoa kiasi cha shilingi billion 4.1 kwa Halamashauri nne zilizokidhi vigezo kuendeleza programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi nchini.
Hafla ya utiaji wa saini wa mikataba ya fedha umefanyika Juni 10, 2022 Jijini Dodoma.
Halmashauri zilizokidhi Vigezo hivyo ni Manispaa ya Kigamboni, Halmashauri ya Wilaya Kishapu, Manispaa ya Lindi na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa(afya)Dkt. Grace Magembe amesema, fedha hizi ni muendelezo wa awamu ya pili kwa Serikali kuzitoa kwa Halmashauri lengo likiwa Halmashauri kuzitumia kama ambavyo zilivyoelekezwa katika mikataba.
Amesema Halmashauri nyingi bado kuna changamoto ya ardhi kwa kutokupangwa na hii hupelekea kutokea kwa migogoro kati ya wananchi na Halmashauri kitu kinachosababisha kuzorotesha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
“Ardhi ikipimwa wananchi wakijenga kwa mpangilio miji yetu itapendeza na kupangwa vizuri na pia ardhi itakua na thamani na tutapunguza migogoro kati ya Halmashauri na wananchi na Serikali itapata mapato” amesema Dkt. Grace
Pia amezielekeza Halmashauri hizo kutumia fedha hizo kama zilivyoelekezwa isitokee fedha hizi kuenda kubadilishwa matumizi.
OR- TAMISEMI kwa kushirikiana na wenzetu Wizara ya Ardhi tutazifuatilia lengo la Serikali mzitumie na kuzirejesha kwa ajili ya Halmashauri nyingine ziweze kufaidika’ alisisitiza.
Awali akisoma hotuba yake Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amesema, katika mwaka wa fedha 2021/22 kupitia programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi Serikali ilishatoa shilingi bilioni 50 kwa Halmashauri 54 nchini na fedha hizo zinapaswa kurejeshwa katika kipindi cha miezi 6.
Akiendelea kufafanua zipo baadhi ya Halmashauri zilizopatiwa mkopo wamepima viwanja lakini mpaka sasa hawajaidhinisha kuuza kwa viwanja, pia amesema zipo Halmashauri wamepatiwa fedha hizo lakini mpaka sasa hawajaanza kuzitumia.
“Halmashauri zilizopatiwa fedha hizo na hawajaanza kutumia kwa lengo waliloombea tutashirikiana na TAMISEMI kuzirudisha ili wapatiwe wengine lakini pia kwa wale wa awali waliopatiwa zinatakiwa kurejeshwa 30 Juni, 2022” amesema Waziri Mabula
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa(USEMI) Bw. Abdallah Chaurembo ameishukuru Serikali kwa kuridhia na kuendelea kutoa mikopo ya fedha kwa Halmashauri na amezitaka Halmashauri kutumia fedha hizo kwa malengo ili kuondoa hoja zinazotokea pindi kamati zinapoeenda kukagua na kujiridhisha kwa matumizi ya fedha walizopokea. Amesisitiza Halmashauri kusimamia programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi iendane na ukusanyaji wa mapato ili kuisaidia Serikali sababu lengo la Serikali ni kuzisaidia Halmashuri kujiendeleza wenyewe
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment