Wamachinga Wapewa Kipaumbele Na Serikali


 Na. Peter Haule, WFM, Dodoma

Waziri wa TAMISEMI, Mhe Innocent Bashungwa, ameitaka sekta binafsi na washirika wa maendeleo kushirikiana na Serikali kuwatengenezea mazingira wezeshi wafanyabiashara ndogo (Wamachinga) ili waweze kukuza biashara zao na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Mhe. Bashungwa ametoa rai hilo jijini Dodoma wakati akifungua warsha ya Machinga iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa ushirikiano na Mfuko wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini (FSDT).

“Wamachinga wakijenjengewa mazingira mazuri yatakayo wawezesha kukuza mitaji yao, ni fursa nzuri kwa Mabenki kwa kuwa yatakuwa na wateja wa kuwakopesha”, alieleza Mhe. Bashungwa

Mhe. Bashungwa aliwataka wadau waliohudhuria katika warsha hiyo kufanya uchambuzi ilikujua maeneo yaliyofanya vizuri kwa wafanyabiashara ndogo (Machinga), changamoto na fursa ili kujua wajibu wa kila mmoja katika kuhakikisha wafanyabiashara hao wanakua na kuleta tija stahiki kwa Taifa

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, alisema kuwa shughuli za machinga zimesaidia kutatua changamoto za ajira kwa vijana kwa kujiajiri na kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alisema kuwa kutokana na umuhimu huo Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa kundi la Wamachinga linahudumiwa kwa upekee kwa kuratibu shughuli wanazozifanya ili ziweze kuwanufaisha na kuwaletea maendeleo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Lawrence Mafuru, alisema kuwa Wizara yake ipo katika hatua za kutengeneza Bajeti Kuu ya Serikali, alisema miongoni mwa vipaumbele katika bajeti hiyo ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan angependa kuviona ni pamoja na sekta ambazo zinazalisha kama Kilimo, mifugo, uvuvi na nishati lakini pia wamachinga.

Amesema kuwa warsha ya wamachinga itasaidia kutoa fursa ya kujifunza lakini pia kuwa na sera itakayoelekeza rasilimali fedha kutoka kwa wadau mbalimbali inapatikanaje kwa ajili ya eneo hilo.

Alisema katika eneo la wamachinga linahudumiwa na wizara nyingi ikiwemo TAMISEMI, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pia katika maeneo ya kiutawala kama Mikoa na Wilaya.

Bw. Mafuru alisema ni vema kuwa na muelekeo mmoja kama Serikali badala ya kulishugulikia suala hilo kwa uelewa wa mtu mmoja mmoja, hivyo warsha hiyo ni muhimu katika kupata maoni ya wadau.

Mwenyekiti wa Wamachinga Taifa, Bw. Ernest Masanja, aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuwakutanisha na wakuu wa mikoa, makatibu tawala na wakuu wa wilaya.

Alisema kuwa kundi la wamachinga lilitengwa lakini sasa linashirikiana vizuri na Serikali hivyo akaahidi wamachinga kuiunga mkono Serikali katika jitihada zake za maendeleo.

Kwa upande wa FSDT wameeleza kuwa wanafuraha kuunga mkono juhudi za ustawi wa wamachinga kwa kuwa ni sekta kubwa na inachangia asilimia 35 katika pato la Taifa.

Warsha hiyo imewakutanisha Makatibu Wakuu wa kisekta, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Idara, viongozi wa wamachinga na wadau wengine.

Mwisho.




from MPEKUZI

Comments