Urusi yachukua udhibiti kamili wa mji wa Mariupol, Ukraine


Russia imetangaza kuchukua udhibiti kamili wa mji muhimu wa Mariupol nchini Ukraine baada ya wanajeshi wa mwisho wa Ukraine waliokuwa katika kiwanda cha chuma cha Azovstal kujisalimisha Ijumaa.

Wizara ya Ulinzi ya Russia imetoa taarifa na kusema kiwanda hicho chote katika mji wa bandarini wa Mariupol kimekombolewa baada ya watu 2,400 waliokuwa hapo, wakiwemo wanachama wa Kikosi cha Wanazi Mamboleo wa Azov kuweka chini silaha na kujisalimisha.

Kabla ya tangazo hilo la Ijumaa la Russia, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine alikuwa amewataka askari wa Ukraine kuondoka katika kiwanda hicho cha chuma ili kuokoa maisha yao.

Rais Vladimir Putin wa Russia amesema wanajeshi wa Ukraine waliojisalimisha watatendewa kwa mujibu wa sheria husika za kimataifa. Wabunge nchini Russia  wanataka wapiganaji wa Kikosi cha Wanazi Mamboleo wa Azov wasichukuliwe kama wafungwa wa kivita bali watangazwe kuwa ni 'wahalifu wa kinazi' na hivyo wasijumuishwe katika ubadilishanaji wafungwa na Ukraine.

Aidha mwendesha mashtaka mkuu wa Russia ametaka mahakama ya juu nchini humo itangaze Kikosi cha Wanazi Mamboleo wa Azov kuwa ni kundi la kigaidi.

Wakati huo huo Jeshi la Russia limeanzisha oparesheni kubwa ya kuchukua udhibiti wa maeneo ambayo bado yanakaliwa kwa mabavu na jeshi la Ukraine katika mkoa wa kusini mashariki mwa Luhansk ambao imejitangazia uhuru.

Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoigu amesema "Jamhuri ya Watu wa Luhansk itakombolewa hivi karibuni."

Inaaminika kuwa Russia ikifanikiwa kuchukua udhibiti wa majimbo ya Luhansk na Donetsk katika eneo la  Donbass kusini mashariki mwa Ukraine, basi itatangaza ushindi katika vita. Kutekwa mji wa Mariupol, iliko bandari kuu ya Donbass iliyo katika Bahari ya Azov ni katika kufanikisha malengo ya Russia ya kudhibiti majimbo hayo mawili ambayo yametangaza kujitenga na Russia.

Mwezi Februari, Russia ilianzisha oparesheni malumu ya kijeshi dhidi ya Ukraine kutokana na kufeli serikali ya Kiev kutekeleza mapatano ya Minsk. Rais Putin alisema pia oparesheni hiyo inalenga kuwaondoa Wanazi Mamboleo nchini Ukraine.




from MPEKUZI

Comments