Tanzania Yapendekeza Mkakati Wa Pamoja Kupambana Na Ugaidi, Majanga AU


 Na Mwandishi wetu, Malabo

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezishauri nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuwa na mpango mkakati wa pamoja katika kupambana na masuala ya ugaidi na majanga ya kibinadamu.

Akitoa pendekezo la Tanzania katika Mkutano wa 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliomalizika jana usiku Malabo, Equatorial Guinea, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) ambaye alimwakilishwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inapendekeza Umoja wa Afrika uwe na mpango mkakati utakaosaidia kuhakikisha kuwa nchi wanachama wanakwenda pamoja lakini pia kusaidiwa kujengewa uwezo wa kupambana na vitendo vya kigaidi.

“Hakuna nchi hata moja inaweza kusema iko salama kwani vikundi vya kigaidi viko sehemu mbalimbali hivyo kwa kutumia mpango mkakati wa umoja na mshikamano ni rahisi kukabiliana na ugadi…..kwa hiyo ujumbe wetu Tanzania kwa (AU) ni kwamba twende pamoja katika kutokomeza ugaidi,” amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Mkutano huo pia umetoa tamko la pamoja la kuimarisha utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyopitishwa miaka mingi pamoja na kuhakikisha Baraza la Amani na Usalama linakuwa na mpango maalum wa kufuatilia nyendo za kigaidi na kuzitokomeza.

“Baraza la Amani na Usalama pia litasaidia katika kuimarisha amani na usalama kupitia ‘stand by force’ ili kuweza kuingilia na kusaidia kuzuia machafuko pindi yanapojitokeza na kutokomeza vitendo kama hivyo vya kigaidi,” aliongeza Balozi Mulamula

Akielezea kuhusu Mkutano wa 15 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali, Balozi Mulamula alisema kuwa Tanzania imeziomba nchi wanachama kuimarisha ushirikiano na utekelezaji wa pamoja wa utoaji wa huduma za kibinadamu ikiwemo tahadhari za mapema ambazo zinahitaji kupitiwa upya, kuendelezwa na kuimarishwa kwa ajili ya kupata utabiri na tafsiri sahihi ya majanga yatakayotokea na kuyafanyia kazi ipasavyo.

Tanzania pia imeuomba Umoja wa Afrika kuwa na ushirikiano na utekelezaji wa pamoja katika utoaji wa huduma za kibinadamu hasa jukumu la kuhifadhi wahamiaji na wakimbizi.

Aidha, mkutano wa 15 na 16 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliridhia kuzizuia nchi nne ambazo kushiriki mikutano ya Umoja wa Afrika kutokana na Mabadiliko ya Serikali yasiyozingatia misingi ya Katiba ikiwemo mapinduzi ya kijeshi nchi hizo ni Mali, Burkina Faso, Guinea na Sudan.

Kwa upande wake, Rais wa Cameroon na Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama, Mhe. Paul Biya amezitaka nchi wanchama wa Umoja wa Afrika kushughulikia masuala ya kigaidi kwa umoja na mshikamano kwani bila kufanya hivyo mambo hayo hujenga na kuchochea itikadi kali hasa miongoni mwa vijana ambao ni idadi kubwa ya watu katika Bara la Afrika.

“Zaidi ya asilimia 60 ya idadi ya watu barani Afrika ni vijana. Kwa hiyo ni lazima nchi wanchama wa Umoja wa Afrika kujitahidi kuweka mazingira mazuri ya ushirikishwaji wa vijana na wanawake katika michakato ya amani na maendeleo katika ngazi ya kitaifa, kikanda na bara,” amesema Mhe. Biya.

Wakuu wa Nchi na serikali katika Mkutano wa 16 wa Dharura waliridhia kwa pamoja kuwa kila mwaka tarehe 31 Januari kuwa siku ya Amani na maridhiano Barani Afrika na Rais wa Angola Mhe. João Lourenço atakuwa kinara ‘champion’ wa masuala ya amani.


from MPEKUZI

Comments