Waziri Mkuu Awataka Watanzania Kutumia Fursa Za Muungano


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wafanyabiashara wa pande zote mbili za Muungano watumie vyema fursa ya kibiashara ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili wajengane kibiashara kabla ya kufikiria kutoka nje.

Amesema kuwa mbali na kuwa na soko kubwa la watu zaidi ya milioni 60 ndani ya Muungano pia kuna soko kubwa zaidi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo mwezi uliopita tu waliikaribisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuwa mwanachama.

 “Lakini pia litumieni vizuri soko la SADC (Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika) pamoja na soko kubwa zaidi la nchi zote 54 za Afrika kupitia African Continental Free Trade Agreement.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumapili, Aprili 24, 2022) alipomuwakiliaha Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango katika Ufunguzi wa Maonesho ya Maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania, yaliyofanyika katika uwanja wa Maisara, Zanzibar.

“Serikali zetu mbili zitaendelea kutekeleza maono ya viongozi wetu ya kuhakikisha changamoto za kifedha na za kikodi za pande za muungano zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili kuchochea ukuaji wa uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na kwa manufaa ya serikali zetu zote mbili”

Aidha, Waziri Mkuu amewataka Watanzania waendelee kujivunia na kuyatangaza mafanikio na maendeleo makubwa yanayotokana na kasi ya viongozi wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi, Rais wa Serika la Mapindizi ya Zanzibar 

Akizungumzia kuhusu ufumbuzi wa hoja mbalimbali za Muungano, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa azma njema ya viongozi wetu imeendelea kusimama imara na kuhakikisha hoja hizo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa maslahi mapana ya muungano wetu.

“Nyote ni mashahidi hivi karibuni tu tumetatuwa changamoto 11 ambazo kwa namna fulani zilikuwa zinakwaza wananchi wetu na bado kazi inaendelea kuzimalizia changamoto zilizobaki.”

Alisisitiza kuwa katika hoja zilizopatiwa ufumbuzi ni pamoja na suala la ajira katika Serikali ya Muungano, ambapo Zanzibar ina asilimia 21 ya ajira zote zinazotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka vijana na Watanzania kwa ujumla waendelee kulinda na kuzienzi harakati za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Uhuru wa Tanganyika ambavyo ndio msingi mkubwa wa Muungano wetu.

“Watu tuendelee kuenzi tunu ya amani na utulivu wa nchi ambayo ndiyo nguzo ya maendeleo tuliyonayo na kwa vizazi vijavyo.”

Awali, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdalla amezishukuru  Wazara,Taasisi na wafanyabiashara kwa kutoa mchango mkubwa katika kuhakikisha  maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano pamoja na Maonesho yaliyofunguliwa na Waziri Mkuu vinafanikiwa.

Alimhakikishia Waziri Mkuu kuwa Wazanzibari wanauthamini Muungano kwani una faida kubwa  kwao na kwa ndugu zao wa Tanzania Bara hivyo wataendelea kuuenzi, kuulinda na kuudumisha.


(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU


from MPEKUZI

Comments