Sababu za Uber kusitisha huduma Tanzania

 Kampuni ya Uber ambayo hutoa huduma ya usafiri ya taxi kwa njia ya mtandao imesitisha huduma zake nchini Tanzania.



Taarifa iliyotumwa na timu ya Uber kwa wateja wa usafiri huo maarufu nchini imesema kuwa wameamua kusitisha huduma zake kuanzia leo Alhamisi 14 Aprili 2022.


Taarifa hiyo ambayo imetumwa kwenye email za wateja jana Jumatano imesema kuwa huduma za UberX, UberXL na UberX Saver hazitapatikana nchini Tanzania.


Taarifa hiyo imeeleza kuwa sababu ya kusitisha huduma hiyo ni kutokana na kanuni za usimamizi wa sekta hiyo kujenga mazingira ambayo si rafiki na zimekuwa changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara hiyo.


 “Tumechukua uamuzi mgumu wa kusitisha kwa muda huduma za UberX, UberXL na UberX Saver nchini Tanzania, bidhaa hizi hazitapatikana kuanzia Alhamis 14 Aprili 2022. Kanuni za sasa za usimamizi wa sekta hii zimejenga mazingira ambayo si rafiki na zimekuwa changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara yetu, hadi pale muafaka utakapopatikana, hatutaendelea kutoa huduma za usafiri wa UberX, UberX Saver na UberXL nchini Tanzania.


"Tunapenda kuchukua fursa hii kukushukuru kwa dhati- kwa kuchagua mfumo wetu kufanya safari zako jijini Dar es Salaam ambako tumekuwa tukitoa huduma zetu kwa kipindi cha miaka sita iliyopita"  imesema taarifa hiyo na kuongeza


“Huu ni wakati mgumu kwetu sote, lakini hii haina maana kwamba ndio mwisho wa kila kitu. Tuko tayari kushirikiana na mamlaka husika na kuwa na mazungumzo yatakayoleta tija na kujenga mazingira wezeshi na tutarudi na kuendelea na kukupa usafiri wa kutegemewa na wa uhakika ambao umekuwa ukiitumia, baada ya kujiridhisha kwamba mazingira ya kibiashara ni rafiki"



from MPEKUZI

Comments