Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeingia makubaliano ya kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kanda, ambacho kipo Nchini Msumbiji.
Akizungumza Aprili 22, 2022 wakati akiwasilisha msimamo wa Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wa dhararua wa Kamati ya Mawaziri wanaohusika na Usimamizi wa Maafa uliofanyika kwa njia ya mtandao Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Mwalimu amesema serikali imeridhia mkataba wa uanzishwaji wa kituo hicho.
Mhe. Ummy alisema lengo la kuanzisha kituo hicho ni kusimamia masuala ya maafa na huduma za kibinadamu kwa Nchi Wanachama zitakazokumbwa na maafa hivyo kitasaidia kuendeleza ushirikiano, kuimarisha uwezo wa Kikanda wa kukabiliana na maafa pamoja na kujenga mazingira rafiki ya shughuli za maendeleo hatimaye kukuza uchumi wa Jumuiya.
“Sisi kama Nchi tumeridhia mkataba huo na tunaipongeza serikali ya Msumbiji kwa kukubali kijengwe katika nchi yao na sisi tutaendelea kushirikiana kama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kinafanya kazi na kutoa taarifa na takwimu katika Ukanda wa Afrika na hata kutoa misaada ya kibinadamu wakati wa majanga,”Alisema. Mhe. Ummy.
Pia aliipongeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika kwa jitihada inazofanya kuimarisha Mfumo wa Usimamizi wa Maafa kwa kushirikiana na Nchi Wanachama.
Aidha alibainisha kwamba serikali ya Tanzania imekubali ombi la msaada wa kibinadamu kwa Nchi ya Afrika Kusini inayohitaji kiasi cha fedha dola za Kimarekeni 300,000 kufuatia majanga ya mafuriko yalitokea nchini humo huku akiomba sekretarieti kuendelea kufuata utaratibu wa utoaji wa fedha hizo ili kusaidia manusura hao.
“Serikali imeunga mkono kuhusu ombi la msaada kwa Jamhuri ya Afrika Kusini kutokana na mafuriko waliyoyapata kule upande wa Kwazulu Nata sisi kama serikali tumeridhia jambo hilo na kuendelea kushauri sekretarieti ifuate utaratibu wa utoaji wa fedha hizo ,”alifafanua Mhe. Ummy.
Awali mkutano huo ulitanguliwa na mkutano wa Makatibu Wakuu kuhusu Usimamizi wa Maafa katika Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika kwa njia ya mtandao ambapo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bwa. Kaspar Mmuya alihudhuria mkutano huo.
===MWISHO===
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment