Mji mkuu wa Ukraine, Kiyv watikiswa kwa mashambulizi makali ya Makombora Ya Urusi


Mji mkuu wa Ukraine umetikiswa kutokana na mashambulio makali yaliyofanywa na majeshi ya Urusi wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akifanya ziara nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa sehemu kadhaa zimepigwa katika mji mkuu, Kiyv kwa mara ya kwanza tangu majeshi ya Urusi yalipoondoka kwenye mji huo wiki zilizopita. Maafisa wanaoshughulikia mambo ya uokozi wamesema watu kadhaa wamejeruhiwa na wengine wamenaswa chini ya vifusi baada ya majengo mawili kuteketezwa.

Mashambulio hayo yalifanyika muda wa takriban saa moja baada ya Rais Zelensky na mgeni wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuzungumza na wandishi wa habari mjini Kiev. Guterres amesema Ukraine imegeuka kuwa kitovu cha maafa yasiyovumilika na ya kuumiza roho. 

Msemaji wa Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa Guterres yupo katika hali salama pamoja na ujumbe wake wote. 

Wakati huo huo milipuko ilisikika nchini Ukraine kote ikiwa ni pamoja na mji wa Polonne uliopo magharibi na kwenye mji wa Chernihiv uliopo karibu na mpaka wa Belarus. Majeshi ya Urusi pia yameupiga kwa makombora mji wa Fastiv ambao ni kituo kikuu cha usafiri wa reli. 

Katika kadhia nyingine idara husika za serikali ya Ukraine zimesema Urusi ilifanya mashambulio makali kwenye jimbo la Donbas. Jimbo hilo la mashariki ndio makao makuu ya viwanda kwenye sehemu hiyo.

 Urusi imesema lengo lake kuu ni kuliteka jimbo hilo. Katika mji wa Mariupol wa kusini mwa Ukraine, wanajeshi wa nchi hiyo waliojibanza ndani ya kiwanda cha chuma bado wanaendelea kupambana.



from MPEKUZI

Comments