Waziri Mulamula Akutana Na Waziri Wa Biashara Na Uwekezaji Wa Saudi Arabia


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Biashara na Uwekezaji Mhe. Dkt. Majid bin Abdullah Al- Qasabi katika Ofisi za Wizara hiyo jijini Riyadh- Saudi Arabia.
 
Waziri Mulamula amemuhakikishia Mhe. Dkt. Al-Qasabi utayari wa Tanzania katika kushirikiana na Saudi Arabia kuptia sekta za mifugo, uvuvi, uwekezaji na usafiri wa anga.
 
Katika ziara hiyo Balozi Mulamula ameambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, Mkurugenzi wa Idara ya Mashriki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Hemedi Mgaza, kaimu Mkurugenzi Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bibi Anna Lyimo na wawakilishi wa wafanyabiashara, wenye Viwanda na Wakulima kutoka Tanzania Bara .
 
Balozi Mulamula na ujumbe wake wanatarajia pia kukutana na viongozi wa Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini humo na wafanyabiashara marafiki wa Tanzania walioko jijini Riyadh.
 
Balozi Mulamula na ujumbe wake pia wanatarajia kukutana na kuzungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara walioko katika miji ya Jeddah na Makkah katika mkutano utakaofanyika jijini Jeddah.
 
Waziri Mulamula na ujumbe wake waliwasili nchini Saudi Arabia kwa ziara ya kikazi tarehe 9 ikiwa ni mualiko uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Mwana Mfalme, Mtukufu Faisal bin Farhan Al Saud, alipotembelea Tanzania mwezi Machi 2021. Balozi Mulamula na ujumbe wake wanatarajia kurejea nyumbani tarehe 13 Machi 2022.


from MPEKUZI

Comments