Waziri Makamba autangaza mradi wa LNG Kimataifa


Houston, Texas

Katika Mkutano wa 40 wa CERAWeek unaofanyika jijini Houston, Marekani Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ameendelea kuitangaza Tanzania na hususani mradi wa LNG unaotarajiwa kujengwa mkoani Lindi, kusini mwa Tanzania. Waziri Makamba alialikwa kama mzungumzaji katika mkutano huo unaojumuisha zaidi ya nchi 100, washiriki zaidi ya 6000 na wazungumzaji zaidi ya 840 kutoka Serikalini na sekta binafsi wanaoshughulika na sekta ya nishati duniani .

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Makamba alisema “Tanzania sasa iko tayari kutekeleza mradi wa LNG na Serikali pamoja na wawekezaji wana nia ya dhati kabisa kuona mradi huu unakamilika ndani ya muda mfupi ili kuanza kuvuna kiasi kikubwa cha gesi asilia kilichopo baharini”.

Waziri Makamba alieleza kuwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Kusini mwa Afrika imepiga hatua kubwa katika ukuaji wa uchumi lakini ili kufikia matamanio ya Serikali na wananchi wake ni lazima kuhakikisha nchi inakuwa na nishati ya uhakika na ya bei stahamilivu.

Waziri Makamba aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kwamba tayari majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji yanaendelea na lengo ni kufikia makubaliano ndani ya mwaka 2022. “Kitu kingine kizuri kuhusu mradi wa LNG Tanzania ni kwamba gesi yetu ina kiasi kidogo sana cha hewa ukaa na hivyo kuwa miongoni mwa gesi ambayo inavutia zaidi wateja duniani kote ukizingatia mikakati ya dunia ya kupunguza hewa ukaa kwa ajili ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi” alieleza zaidi Waziri Makamba.

Mojawapo ya mada kuu ya mkutano wa 40 wa CERAWeek ni kuhusu mabadiliko ya matumizi ya nishati kutoka nishati zenye kutoa hewa ukaa nyingi kuelekea nishati zenye kutoa kiasi kidogo cha hewa ukaa ikiwa ni mikakati ya kidunia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Waziri Makamba alieleza baadhi ya mikakati na hatua ambazo Tanzania inachukua katika kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa ikiwemo kuchochea matumizi ya gesi asilia katika magari, matumizi ya gesi asilia kuzalisha umeme na kuondokana na matumizi ya mafuta mazito na pia matumizi ya gesi za mitungi kwa ajili ya kupikia.

“Asilimia 60% ya umeme katika gridi ya Taifa inazalishwa na gesi asilia huku asilimia 40% iliyobaki inatokana na vyanzo vingine ambavyo ni rafiki kwa mazingira ikiwemo maji” alisema Waziri Makamba. Waziri Makamba aliongeza kuwa bado kuna changamoto ya kuhakikisha matumizi ya kuni na mkaa yanapungua na ili kufanikisha hili ni lazima wananchi wapatiwe vyanzo mbadala vya nishati ambavyo vinaendana na kipato chao na uhalisia wa maisha yao.

Katika mkutano huo Waziri Makamba ameambatana na viongozi kutoka Wizara ya Nishati akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Ndg. Kheri Mahimbali, Kamishna wa Gesi na Mafuta, Ndg. Michael Mjinja, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio, Mkurugenzi Mtendaji wa EWURA, Mha. Godfrey Chibulunje, Mkurugenzi Mtendaji wa PURA, Mha. Charles Sangweni pamoja na maofisa wasaidizi wa viongozi.



from MPEKUZI

Comments