Wahukumiwa Miezi Sita Baada Ya Kufanyiana Usaili Wa Kuandika Unaoratibiwa Na Sekretarieti Ya Ajira Katika Utumishi Wa Umma


Mahakama ya Wilaya ya Dodoma imewatia hatiani waombaji kazi wawili Mabula Edward Kanga  pamoja na Joel Johnson Kimatare baada ya kufanya udanganyifu wakati wa zoezi la usaili kwa nafasi za Uhandisi Ujenzi uliofanyika tarehe 08 Mei, 2021 katika Ukumbi Wa Chuo Kikuu cha UDOM.

Kutokana na umakini unaofanywa na Watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma wakati wa uratibu wa michakato ya ajira, walifanikiwa kumkamata msailiwa Joel Johnson Kimatare ambaye alifika katika eneo hilo kwa ajili ya kumfanyia usaili Bwana Mabula Edward Kanga.

Mabula Edward Kanga aliitwa kufanya usaili 8/5/2021 uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma kwa nafasi ya Mhandisi-Ujenzi kwa ajili ya taasisi ya Watumishi Housing Company na badala yake akamtuma Joel Johnson Kimatare kumfanyia usaili huo akitambua ni kosa kisheria. Ndugu Joel Johnson Kimatare alipofika kufanya usaili, alikaguliwa vyeti na kuhurusiwa kuingia ndani ya chumba cha usaili wa kuandika na kwa makusudi alikwenda kukaa pasipo kujisajili kwenye orodha ya wasailiwa akihofia kukamatwa.

Baada ya usaili, maofisa wa Sekretarieti ya Ajira walihakiki idadi ya wasailiwa waliojisajili kabla ya usaili na idadi ya wasailiwa baada ya usaili na kubaini uwepo wa msailiwa mmoja ambaye hakuwa amejisajili. Maofisa hao walimtaka msailiwa ambaye hakuwa amejiandikisha asimame ili ahudumiwe na ndipo Bwana Joel Johnson Kimatare alisimama na kujitambulisha kwa jina la Mabula Edward Kanga. Alipotakiwa kutoa vyeti vyake na kitambulisho, ndipo ikabainika kuwa yeye anaitwa Joel Johnson Kimatare na sio Mabula Edward Kanga. Baada ya kukamatwa, mtuhumiwa Joel Johnson Kimatare alichukuliwa na jeshi la polisi na kufunguliwa kesi iliyohitimishwa tarehe 28 Februari, 2022 katika mahakama ya Wilaya ya Dodoma kwa kuwatia hatiani watuhumiwa wote wawili.

Kesi hiyo ya jinai Na. 46 ya Mwaka 2021 ilifunguliwa kwenye Mahakama ya Wilaya ya Dodoma tarehe 16 Mei 2021 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi D.J Mpelembwa na watuhumiwa walikutwa na hatia baada ya mahakama kujiridhisha na maelezo ya mashahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani.

Akitoa ushahidi wake, Naibu Katibu anayesimamia masuala ya TEHAMA na ambaye kwa sasa ni Kaimu Katibu wa Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Mhandisi Samwel Tanguye aliieleza mahakama kuwa yeye ni Msimamizi wa Mfumo wa Ajira portal ambao umemtambua Mabula Edward Kanga kuwa ndiye aliyeomba kazi za Uhandisi Ujenzi kwa ajili ya Watumishi Housing company na kwamba namba ya usaili ilitumwa kwenye akaunti yake. Hivyo, ni dhahili kuwa wawili hao waliwasiliana ili kuweza kupeana namba za usaili ambazo Joel Johnson Kimatare alizitumia wakati wa usaili wa kuandika.  Pia, Afisa Utumishi wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Bwana Ally Mnyimwa aliieleza mahakama kuwa, alimruhusu Ndg. Joel Johnson Kimatare kuingia ndani ya chumba cha usaili baada ya kumkagua vyeti mlangoni kabla ya Joel kuwakwepa maofisa waliokuwa wakikagua vitambulisho kabla ya kuwasainisha kwenye karatasi ya mahudhurio na kwenda kuketi kusubiri kufanya usaili wa kuandika.

Baada ya Mahakama kuwatia hatiani watuhumiwa wote wawili, Mwendesha mashtaka wa Serikali Mhe. Meshack Lyabonga aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa watuhumiwa ili iwe fundisho kwa wengine kwani vitendo hivyo vinatia aibu kwa vijana wasomi katika jamii yetu.

Katika kesi hiyo, Washitakiwa wote wawili walikiri kufanya makosa hayo na kuiomba mahakama iwasamehe kwa kuwa ilikuwa ni mara yao ya kwanza kufanya kosa hilo.   Mtuhumiwa wa kwanza ambaye ni Mabula Edward Kanga baada ya kutiwa hatiani, aliiomba mahakama imhurumie kwani anao watoto wanne na wote wakimtegemea na mtuhumiwa wa pili Joel Johnson Mabula aliiomba mahakama imruhumie kwani alikuwa akimuuguza mama yake mzazi.

Tarehe 28/02/2022 Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Dodoma ilitoa hukumu ya kifungo cha nje miezi sita kwa washitakiwa wote wawili. Aidha, Hakimu Mkazi Mwandamizi D.J Mpelembwa amewataka kutokufanya makosa ndani ya kipindi hicho cha miezi sita tangu kutolewa kwa hukumu hiyo.

Kaimu Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Mhandisi Samwel Tanguye amewaasa waombaji fursa za ajira nchini kuacha tabia ya udanganyifu wakati wa michakato ya ajira kwani inaweza kuwaondolea sifa za kuajiriwa ndani ya utumishi wa umma. Kwa mujibu wa Kaimu Katibu huyo, Ndg. Mabula Edward Kanda na Joel Johnson Kimatare wamepoteza sifa za kuajiriwa katika Utumishi wa Umma.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

OFISI YA RAIS SEKRETARIETI YA AJIRA KATIKA UTUMISHI WA UMMA



from MPEKUZI

Comments