Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifaya mauaji ya wazee watatu (Agnes Msengi miaka 84, Windila Saidi miaka 80 na Winfrida Gigila miaka 80) waliouwawa kwa kuchomwa moto na wanakijiji wenzao kwa kile kinachodaiwa kuwa wamekuwa wakishiriki vitendo vya kishirikina. Tukio hilo lilitokea tarehe 27/03/2022 katika kijiji cha Kisharita wilayani Iramba mkoani Singida.
Vitendo hivyo ni ukatili mkubwa ambao Serikali haiwezi kuvumilia na ni kinyume na sheria za nchi yetu na hata maagizo ya Mwenyezi Mungu katika dini zote zinapinga ukatili huu.
Serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuchukua hatua za kutokomeza vitendo vya Ukatili hapa nchini kwa kusimamia utekelezaji wa; Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18-2021/22), Mkakati wa kutokomeza mauaji dhidi ya Wazee 2018/19 – 2022/2023, Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 20, Sera ya wazee 2003, na Uundwaji wa Mabaraza ya Wazee kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa, Kata, Wilaya, Mikoa na Taifa.
Pamoja na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na vyombo vya dola, nawaagiza Maafisa Ustawi wa Jamii na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwa karibu na wananchi ili kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuweza kuzitatua kwa wakati ikiwemo kuwaelimisha fursa zilizopo za kujikwamua kiuchumi, kuondokana na msongo wa mawazo na kukemea mila na desturi zinazochochea vitendo vya ukatili.
Pia nawasisitiza wazee wote nchini kupitia Mabaraza yao katika ngazi ya Vijiji/Mtaa na Kata kutoa taarifa za viashiria vyovyote vinavyohatarisha usalama wa wazee katika maeneo yao ili kuzuia vitendo vya ukatili.
Mwisho niiombe jamii, wanapoona matukio au viashiria vya vitendo vya ukatili watoe taarifa mapema kwa mamlaka zinazohusika kwa msaada wa haraka ili tuweze kuokoa maisha ya Wananchi wasio na hatia.
Imetolewa na:
Mhe. Dkt. Dorothy O. Gwajima (Mb)
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment