Mganga Mkuu Wa Serikali Awataka Wananchi Kubadili Mtindo Wa Maisha Ili Kukabiliana Na Ugonjwa Wa Figo


NA WAF- KIBAHA

MGANGA Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe ametoa wito kwa Watanzania kubadili mtindo wa maisha ikiwemo suala la ulaji unaofaa, kupunguza unywaji wa vileo, kuepuka uvutaji wa sigara, kuepuka kula vyakula vya mafuta mengi na chumvi pamoja na kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Figo.

Dkt. Sichalwe amesema hayo  Machi 9, 2022 katika maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani yaliyofanyika Kitaifa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tumbi – Kibaha Mkoa wa Pwani.

“Naomba nikumbushe umuhimu wa kubadilisha mtindo wa maisha kwa kuhimiza ufanyaji wa mazoezi,kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, kupunguza unywaji wa pombe, vile vile kuzingatia ulaji wa mlo kamili wenye mboga mboga na matunda ili kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa.” Amesema.

Amesema, kupitia utafiti uliofanyika mwaka 2013 katika jamii ulionesha kuwa asilimia 7 ya watanzania wanaishi na ugonjwa wa Figo, huku akiweka wazi kuwa Wagonjwa wengi wenye tatizo la Figo pia walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa kisukari na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Aidha, Dkt. Sichalwe amesema, Hadi kufikia  Januari 31, 2022 wagonjwa 2750  sawa na asilimia 32%  wamepata huduma ya kusafishwa damu (dialysis) na  wagonjwa 325 wamepandikizwa Figo.

Sambamba na hilo Dkt. Sichalwe amesema, tafiti zimebaini kuwa, takriban Watanzania 5800 mpaka 8500 wanahitaji huduma ya kusafisha damu yaani (dialysis) au huduma za kupandikizwa figo.

“Tafiti zimebaini kuwa takriban Watanzania 5800 mpaka 8500 wanahitaji huduma ya kusafisha damu yaani ‘dialysis’ au huduma za kupandikizwa Figo.”Amesema.

Hata hivyo, amewataka wazi kuwa, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeanzisha awamu ya pili ya upanuzi wa huduma za uchujaji damu kwa wagonjwa wa Figo ‘dialysis’ katika hospitali nyingine 12 nchini, huku mashine za dialysis 110 na mashine za kuchakata maji 11 zimeanza kusimikwa katika hospitali husika.

Amesema mipango iliyopo ni kwamba Ifikapo Juni, 2023 hospitali zote za Rufaa nchini zitakuwa zikitoa huduma za usafishaji damu (dialysis) na hivyo kusogeza huduma hii karibu na wananchi, hivyo kuongeza kiwango cha watu wanaofanyiwa dialysis kutoka asilimia 32 ya sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo June 2023,” amesisitiza.

Naye,Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Sara Msafiri amesema kuwa, mpaka sasa tayari wananchi 1200 wameshapima afya zao tangu maadhimisho haya yalipoanza siku ya Machi 7, huku akiweka wazi zaidi ya wananchi 600 tayari wameshajiandikisha ili kupata huduma za uchunguzi, hivyo kumwomba Mganga Mkuu kuongeza siku ili wananchi waendelee kunufaika na huduma hiyo.

Amesema, taarifa zinaonesha kuwa, kati ya wananchi 1200 waliofanya huduma ya upimaji afya, wananchi 100 wamegundulika kuwa na ugonjwa au kuwa na viashiria vya ugonjwa wa figo, hivyo kuahidi kuendelea kutoa Elimu ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa huduma za tiba kutoka Wizarabya Afya Dkt. James Kihologwe amesema, takriban zaidi ya asilimia 64 ya watu wenye tatizo la kisukari hawajitambui kama wanatatizo la kisukari mpaka wanapoenda kufanya uchunguzi, na kisukari ni moja ya sababu ya kupata ugonjwa wa figo.

Zaidi ya robo tatu ya watu wenye tatizo la shinikizo la damu, hawajifahamu kama wana tatizo hilo, mpaka wanapoenda kufanya uchunguzi, jambo ambalo hupelekea kupata madhara ya figo, amesisitiza Dkt. Kihologwe.



from MPEKUZI

Comments