Na Mwandishi wetu, Dar es salaam
Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari imekutana Jijini Dar es Salaam kujadili uanzishwaji wa Mfumo wa kuzuia migogoro nchini ili kurahisisha shughuli za uratibu wa kamati hiyo.
Akifungua kikao cha kamati hiyo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene amepongeza kuanzishwa kwa mfumo huo hapa nchini ambao utasaidia kutambua dalili za awali katika matukio yanayoweza kusababisha kutokea mauaji ya kimbari.
“Naishukuru UNDP kwa kubuni wazo la kuanzishwa kwa mfumo huo, kwani kutambua dalili za awali za matukio yanayoweza kusababisha kutokea kwa mauaji ya kimbari kutasaidia sana kuepusha kutokea kwa mauaji hayo siyo tu hapa nchini bali hata kwa nchi nyingine wanachama wa jumuiya yetu, ni wazo zuri na wadau wamelipokea vizuri,” amesema Mhe. Simbachawene.
Amesema Serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha ofisi kwa ajili ya kuratibu mauaji ya kimbari hapa nchini kwa ajili ya kusaidia harakati za kuzuia kutokea kwa mauaji ya kimbari kupitia mfumo huo.
Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameipongeza Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari ambayo imekuwa ikichukua hatua za kuwakutanisha wadau mbalimbali katika jamii kama viongozi wa dini na jumuiya mbalimbali ili kutatua changamoto pale zinapotokea katika jamii nchini.
“Mimi kama mlezi wa kamati nimefarijika kuiona kamati hii ikitekeleza majukumu yake kwa ufanisi na siyo tu kuisaidia Tanzania bali hata nchi nyingine katika ukanda wa maziwa makuu,” amesema Balozi Mulamula.
Balozi Mulamula amepongeza Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa kushirikiana na Serikali ya Uswisi kwa kuona umuhimu wa Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari na hivyo kwa pamoja kuja na mpango wa kuanzishwa kwa kituo ambacho kitakuwa kinatoa taarifa za awali pale vinapokuwepo viashira vya matatizo au hata mauaji ya kimbari na kuongeza kuwa Serikali inaunga mkono jitihada hizo kwani zitaiwezesha kuzuia migogogo ambayo inaweza kusababisha kutokea mauaji ya kimbari nchini.
Kamati ya Kitaifa ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari nchini iliundwa mwezi Februari, 2012 baada ya Tanzania kusaini na kuridhia Itifaki ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliyoridhiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mkataba wa nchi za Maziwa Makuu wa Usalama, Utulivu na Maendeleo.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment