Kamati Ya Bunge Yasifu Mpango Wa Matumizi Ya Ardhi Singidai


Na Munir Shemweta, WANMM SINGIDA

 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imesifu Mpango wa Matumizi ya Ardhi pamoja na upimaji ardhi uliofanyika kwenye vijiji vya Ntondo na Nkwea vilivyopo halmashauri ya wilaya ya Singida katika mkoa wa Singida.

 

Halmashauri ya wilaya ya Singida ina jumla ya vijiji 84 kati ya vijiji hivyo vijiji 20 vinapitiwa na Mkuza wa Bomba la Mafuta na Mipango ya Matumizi bora ya ardhi imeandaliwa katika vijiji 16 kati ya 20 na kufanya jumla ya vijiji 50 katika wilaya ya Singisa kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi.

 

Aidha, Kamati imeitaka Wizara ya Ardhi kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishajj ardhi kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kufikia mwaka 2025 iwe imetimiza malengo na matakwa ya Wizara na kuboresha sekta ya ardhi ili kuiwezesha serikali kuinua uchumi.

 

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge katika vijjiji vya Ntondo na Nkwea tarehe 15 Machi 2022 Mwenyekiti wa Kamati  hiyo Ally Makoa alisema, kiasi cha fedha kilichotolewa kwa kazi za upangaji na upimaji ardhi katika vijiji hivyo imeleta  tija na kutimiza kiu ya Wizara pamoja na ilani ya Chama cha Mapinduzi.

 

"Tunamshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuridhia shilingi Bilioni 50 kuja katika mpango wa kupanga kupima na kumilikisha ardhi, tunaishukuru Wizara ya Ardhi kwa kujituma na kuandaa hati. Fedha zilizotolewa na serikali kupitia Wizara ya Fedha zinajibu matarajio ya ilani ya ccm" alisema Makoa

 

Kwa mujibu wa Makoa, kamati yake inatamani maeneo yote yaliyozingatiwa kwenye mipango ya upangaji na upimaji yanazingatiwa kwa kuwekewa alama zinazoonesha mipaka na matumizi ya maeneo ili kuepuka uvamizi unaoweza kufanywa na baadhi ya watu.

 

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt Benelith Mahenge ameiomba kamati na Waziri wa Ardhi kusaidia halmashauri za mkoa wake kuongezewa bajeti ya kupanga na kupima maeneo katika halmashauri hizo.

 

Akizungumza mbele ya Kamati  hiyo Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula  aliipongeza kamati ya Bunge kwa maoni na ushauri wanaoutoa mara kwa mara na kuekeza kuwa ushauri na maoni umesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta  ufanisi katika utekelezaji majukumu ya wizara.

 

Aidha, alisema katika mwaka huu wa fedha 2021/2022  mradi wa upangaji matumizi ya ardhi uliidhinishiwa jumla ya shilingi Bilioni 1:5  na hadi kufikia Februari 2022 shilingi milioni  844.5 zilikuwa zimepokelewa "

 

"Utekekezaji mradi wa upangaji matumizi ya ardhi umewezesha vijiji 239 vilivyopitiwa na miradi ya kimkakati kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi"

 

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, Wizara ya Ardhi  inaendelea kutekekeza program ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi na amemshukuru rais Samia kwa kutupatia bilioni 50 kwa mara moja jambo ambalo halijawahi kufafanyika katika kipindi kifupi"

 



from MPEKUZI

Comments