Balozi Wa Uingereza Nchini Tanzania Aridhishwa Na Utendaji Kazi Wa Rais Samia.


BALOZI wa Uingereza nchini, amesifu uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia  demokrasia hapa nchini ikiwa ni mwaka mmoja tangu aingie madarakani.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Mwanza, Balozi David Concar, alisema nchi yake inaridhishwa na hali ya siasa inavyoendelea kwa sasa hapa nchini.

Alisema suala la kuwapo demokrasia limeimarika ndani ya mwaka mmoja  na kwamba wataendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Alisema nchi yake itaendelea kushirikiana  na Tanzania katika nyanja mbalimbali  za kiuchumi kwa manufaa ya  nchi hizo mbili.

Aliongeza kuwa  kwa sasa uhuru wa vyombo vya habari umeimarika ndani ya mwaka mmoja wa utawala wa Rais Samia, huku akishauri waandishi wa habari mkoani Mwanza  (MPC) kuweka mpango kazi ili kuandika habari zinazohusu wanawake na watoto.

''Ni vyema MPC  kwenye mpango kazi wenu ikaweka jukumu la kuripoti habari zinazohusu usawa wa kijinsia na haki za wanawake na watoto,'' alisema balozi huyo.

Kuhusu mzozo wa nchi za Ukraine na Urusi, alisema nchi itaendelea kujikita kutoa misaada ya kibinadamu na inaamini kwamba uvamizi huo haukuwa wa haki.

Kutokana na hali hiyo, balozi Concar alisema mataifa mengi yalipaza sauti zao kupinga Urusi kuvamia Ukraine  na kumtaka Rais Vladmir Putin kusitisha vita hiyo.

Kwa upande wao, baadhi ya waandishi wa habari mkoani Mwanza, walimshukuru, balozi huyo kwa nchi yake kuwa na programu maalum ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari.




from MPEKUZI

Comments