TANESCO na ZECO Zaanza Mchakato wa Kuongeza laini ya kutoka Kunduchi mpaka Mtoni Zanzibar itakayopitisha megawati 200


 Immaculate Makilika – MAELEZO, Zanzibar
Shirika la umeme Tanzania TANESCO pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) yameendelea kushirikiana kwa karibu na kwenye upande wa usafirishaji na biashara ya nishati ya umeme nchini.

Ikiwa ZECO ni moja ya wateja wakubwa na muhimu kwa TANESCO ikitajwa kuchangia sehemu kubwa ya mapato ya TANESCO kiasi cha takribani shilingi billion 91.7 za kitanzania kwa mwaka.

Akizungumza  Februari 13, 2022, Visiwani Zanzibar, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa ya wiki kuhusu utekelezaji wa miradi ya Serikali katika maeneo mbalimbali nchini alisema, “Mhe. Rais Hussein Ali Mwinyi amekuja na msisitizo wa uchumi wa Buluu ambao utahitaji matumizi makubwa ya umeme kwa ajili ya viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji, ambapo tayari kumeshaonekana dalili za kuongezeka kwa matumizi ya umeme Zanzibar.

Hivyo, ili kuendana na juhudi hizo za Mhe. Rais, TANESCO na ZESCO zimeanza mchakato wa haraka wa kuongeza laini nyingine (marine cable) kutoka Kunduchi mpaka Mtoni Zanzibar itakayopitisha megawati 200”.

Msigwa alisisitza “TANESCO imeendelea kuihudumia Zanzibar vizuri kupitia njia za umeme zilizovushwa baharini kuna, njia ya kutoka Kunduchi kuja hapa Zanzibar ambapo kuna laini mbili za msongo wa kilovolti 132 (marine cable) ya kwanza ina uwezo wa megawati 50 na ya pili megawati 100, njia hizi ndizo zinaleta umeme hapa Unguja ambapo mahitaji yake ni megawati 93.4 mpaka sasa.”

Aliongeza kuwa kutoka Tanga kuna njia ya msongo wa kilovoti 33 (marine cable) kwenda Pemba yenye uwezo wa megawati 20 ambapo matumizi makuu hadi sasa kwa upande wa Pemba ni megawati 13.



from MPEKUZI

Comments