Tamisemi Chunguzeni Matumizi Ya Fedha Za Miradi-Majaliwa


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI afanye uchunguzi wa matumizi ya fedha za miradi ya UVIKO-19 na miradi mingine na kuchukua hatua za kinidhamu kwa viongozi na watendaji wote watakaobainika kufanya ubadhirifu.

Mheshimiwa Majaliwa amechukua hatua hiyo baada ya baadhi ya Halmashauri nchini kubainika kuwa na matumizi yasiyoridhisha ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali hususan miradi ya UVIKO-19.

Ametoa agizo hilo jana (Ijumaa, Februari 18, 2022) wakati akiahirisha Mkutano wa Sita wa Bunge la 12 Bungeni Jijini Dodoma. Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kusisitiza kwamba hatua kali ziendelee kuchukuliwa dhidi ya wote wanaobainika kufanya ubadhirifu.

“Kutokana na taarifa za ubadhirifu mkubwa katika baadhi ya Halmashauri, Serikali itapeleka timu maalumu ya uchunguzi ili kujiridhisha na matumizi ya fedha za umma.”

Pia, Waziri Mkuu ameendelea kuwasisitiza Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa matumizi ya fedha na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha miradi hiyo inaakisi thamani ya fedha za Watanzania.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kutekeleza kwa mafanikio makubwa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 wenye thamani ya shilingi trilioni 1.3.

Amesema utekelezaji wa mpango huo, unaimarisha upatikanaji sambamba na kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi ambapo hadi kufikia Januari 2022, shilingi bilioni 599.7 zimetolewa kwa upande wa Tanzania Bara kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Mpango huo.

Mheshimiwa Majaliwa ameongeza kuwa shilingi bilioni 231 ikiwa ni sehemu ya shilingi trilioni 1.3, zimepelekwa Zanzibar kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya aina hiyo.  “Na sehemu kubwa ya fedha hizo zimetumika kupunguza msongamano wa wanafunzi kwa kuongeza madarasa.

Amesema jumla ya madarasa 12,000 yamejengwa katika shule za sekondari huku madarasa 3,000 yakijengwa katika vituo shikizi na mabweni 50 kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu. Kitendo hiki ni utekelezaji wa vitendo wa utoaji haki na usawa katika upatikanaji wa elimu nchini.

“Ujenzi huo wa vyumba vya madarasa umewezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 na kuondoa changamoto ya kuwepo kwa chaguo la pili yaani second selection na wakati mwingine chaguo la tatu.”

Waziri Mkuu amesema sekta zilizopata fedha hizo hadi Desemba 2021 ni Afya shilingi bilioni 180.4; Elimu shilingi bilioni 353.4; Maji shilingi bilioni 32.7; Utalii shilingi bilioni 26.8; na uwezeshaji wa kaya maskini kupitia TASAF shilingi bilioni 5.5.

Amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa kuzingatia mipango kazi ya mafungu husika, taratibu za maombi ya fedha na mikataba ya kazi zinazokusudiwa kutekelezwa. “Nitoe wito kwa viongozi na watendaji wote wa sekta husika kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi husika ili ikamilike katika muda uliopangwa.”

“Waswahili hunena mwenye macho haambiwi tazama. Sote tu mashuhuda wa mafanikio hayo sambamba na maeneo mengine ambayo kiuhalisia yanaakisi kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa nia ya kuwaletea maendeleo Watanzania.”

Hivyo, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa Watanzania wote bila kujali kujali itikadi zao waendelee kumuunga mkono kwa moyo wa dhati Mheshimiwa Rais Samia ili aweze kutimiza azma yake ya dhati ya kujenga uchumi imara, shindani na endelevu.


from MPEKUZI

Comments