MBUNGE wa Viti Maalum (CCM) Bahati Ndingo ameihoji serikali Bungeni kuhusu mpango uliopo wa kutenga fedha za ukarabati wa vituo vya wazee ambavyo vingi vimechakaa.
Bahati aliuliza swali hilo jana Bungeni kwa Naibu Waziri, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum, Mwanaidi Ali Khamisi.
Akijibu swali hilo, Mwanaidi alisema katika kuboresha utoaji wa huduma, serikali imeendelea kuboresha majengo na miundombinu ya makazi ya wazee kwa awamu ambapo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 na mwaka wa fedha 2020/2021 ukarabati umefanyika katika makazi saba ya wazee yakiwemo Nunge (Dar es Salaam), Kolandoto (Shinyanga), Njoro (Kilimanjaro), Magugu (Manyara), Kiilima (Kagera), Fungafunga (Morogoro) na Sukamahela (Singida).
Aidha, alisema serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Makazi ya Wazee Wasiojiweza nchini kwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha.
Hata hivyo, Mbunge Bahati alipata nafasi kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza ambapo katika swali lake la kwanza alitaka kufahamu mpango wa serikali wa kuongeza idadi ya vituo vya kulelea wazee.
“Tafiti mbalimbali zimeonyesha uwepo wa ongezeko la wazee duniani, je, wizara inajipangaje kuongeza idadi ya vituo vya kulelea wazee,” alihoji.
Kadhalika, katika swali lake la pili, alihoji mpango wa serikali wa kuweka vifaa tiba katika vituo mbalimbali vya kulelea wazee.
Akijibu maswali hayo, Mwanaidi alisema kila mwaka wa fedha serikali imekuwa ikitoa fedha kuboresha mahitaji ya wazee kama mavazi, chakula na afya bora.
Alisisitiza kuwa serikali ya Rais Samia inawajali na kuwathamini wazee kwa kuhakikisha kundi hilo muhimu linapata huduma bora.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment