Jeshi La Polisi Lapigwa Msasa Kukabiliana Na Makosa Ya Uhalifu Wa Mtandao


Na Mwandishi wetu, Dodoma
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetoa mafunzo ya makosa ya mtandao kwa wapelelezi na askari wa chumba cha mashtaka wa jeshi la Polisi Tanzania ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali katika kupambana na makosa ya uhalifu mtandaoni kwa kuwajengea uwezo wataalam wanaoshughulikia masuala ya matumizi salama mtandao na makosa ya uhalifu mtandaoni ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). 


Akifungua mafunzo hayo jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa zoezi la kuwajengea uwezo wataalam katika makundi mbalimbali ni endelevu ili wataalamu hao waweze kuitafsiri na kuifanyia kazi Sheria ya usalama mtandao ya mwaka 2015, kuendana na kukua kwa teknolojia na matumizi ya TEHAMA nchini.


Amesema kuwa kutokana na kukua kwa TEHAMA, uhalifu mwingi unafanywa kwa njia ya mtandao, hivyo ni muhimu kuwajengea uwezo vijana wa jeshi la polisi ili kuwa na jeshi la kisasa katika kupambana na makosa ya uhalifu mtandaoni lengo likiwa ni
Mhandisi Kundo amesisitiza elimu sahihi ya matumizi salama ya mtandao itolewe kwa wananchi katika mazingira yote kupitia vipindi vya televisheni na redio jamii kwa kuitafsiri sheria ya usalama mtandao inayotambulisha makosa na adhabu zake, kwa lengo la kuendelea kujenga imani ya wananchi kwa jeshi la polisi hasa ofisi ya mashtaka ili ofisi hiyo iwe kimbilio la wananchi wanapopata tatizo la uhalifu mtandaoni


Ameongeza kuwa elimu itakayotolewa itasaidia kutoa uelewa kwa wananchi kuwa ofisi inayoshughulikia kesi za uhalifu mtandaoni ipo chini ya jeshi la polisi na sio Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama wananchi wengi wanavyodhani kwa kuwa TCRA inawajibika na usajili na usimamizi wa vifaa vya TEHAMA na huduma za mawasiliano hivyo jeshi la polisi linashirikiana na Mamlaka hiyo kisheria ili kuweza kumtambua mhusika aliyetumia kifaa cha TEHAMA na au huduma za mawasiliano kufanya uhalifu mtandaoni


“Wimbo wa Jeshi la Polisi mlioanza nao ni Mkataba kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, na umetamka bayana majukumu ya jeshi la polisi na kusimika misingi ya uzalendo kwa nchi, nendeni mkautafsiri wimbo huo katika uhalisia”, amezungumza Mhandisi Kundo


Akimwakilisha Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Kamisha Msaidizi wa polisi mwandanizi (SACP) Deusdedit Nsimeki amesema kuwa dunia inabadilika kila siku kwasababu ya kukua kwa teknolojia ambayo pia inachangia kuongezeka kwa makosa ya uhalifu kwa njia ya mtandao, hivyo mafunzo hayo yanatarajiwa  kuongeza tija kwa jeshi la polisi katika kushughulikia makosa ya uhalifu mtandaoni


Naye Shabani Hiki, Kamishna wa Polisi uchunguzi wa kisayansi (CP FB) ameishukuru Wizara kwa kulitendea haki jeshi la polisi kwa kuandaa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo wataalam wa jeshi la polisi kwasababu lawama nyingi za wananchi kwa jeshi hilo yanaanzia katika chumba cha mashtaka hivyo mafunzo hayo yatasaidia kupunguza malalamiko kwa jeshi la polisi Tanzania kwa upande wa mashtaka yote ya uhalifu mtandaoni


Mafunzo ya kukabiliana na makosa ya uhalifu mtandaoni yanaendeshwa katika maeneo tofauti ya Dodoma,  Dar es Salaam na Morogoro, ambapo wataalamu zaidi ya 400  wanapatiwa mafunzo yanayohusu Upelelezi wa Makosa ya Kimtandao, Ubobezi katika Tathmini ya Usalama wa mifumo na Sayansi ya kiuchunguzi katika mitandao, Matumizi ya moduli ya uhalifu mtandao, Uandaaji wa Mwongozo wa Upelelezi na Uendeshaji wa Mashtaka kwa Mashauri ya Kimtandao, sheria za kuzuia uhalifu mtandao pamojua na ujuzi wa uchunguzi na uendeshaji mashtaka.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI.




from MPEKUZI

Comments