Jaji Mkuu Prof Juma: Dhibitini Ucheleweshaji Wa Mashauri


Na Mary Gwera, Mahakama-Arusha

Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wametakiwa kudhibiti ucheleweshaji wa mashauri mahakamani ili kuhakikisha kuwa haki inapatikana kwa wakati.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi cha Majaji Wafawidhi  tarehe 10 Februari, 2022 jijini Arusha, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wamechangia utekelezaji wa Dhima ya Mahakama ya Tanzania ya Upatikanaji wa Haki kwa wote na kwa wakati.

“Ninyi ni Viongozi na pia ni watu muhimu sana katika utekelezaji wa sheria hivyo mnatakiwa kuwa mstari wa mbele kusimamia suala la uondoshaji wa mashauri kwa wakati pamoja na kufanya uboreshaji wa huduma za Mahakama kwa ujumla,” alisema Mhe.Prof. Juma.

Aliainisha baadhi ya mashauri yanayolalamikiwa kucheleweshwa kuwa ni Mashauri ya Mirathi na Mashauri ya Jinai huku akiwasisitiza Waheshimiwa Majaji kufanya jitihada binafsi katika Kanda wanazosimamia ili kuwezesha kumaliza mashauri kwa wakati.

“Ni muhimu kuzingatia mikakati ya Taasisi kuhusu uondoshaji wa mashauri, mbali na mikakati hii ni rai yangu kwenu Majaji Wafawidhi kuwa na mikakati binafsi ya kikanda ambayo inalenga kuboresha zaidi utoaji wa haki kwa wakati,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.

Aliongeza kuwa Jaji Mfawidhi ni Msimamizi Mkuu katika Kanda au Divisheni hivyo basi,panapotokea mabadiliko ya sheria au Kanuni zinazogusa shughuli za utoaji haki, ni wajibu wa Jaji Mfawidhi kuyaelewa mabadiliko hayo mapema na kuwaelimisha watumishi wote kuhusu mabadiliko hayo.

“Huwezi kufanikiwa katika nafasi yako ya Jaji Mfawidhi endapo huielewi Tanzania na mazingira mbalimbali yanayoizunguka Tanzania (Understanding the context of the United Republic of Tanzania; Context of Separation of Power; Regional Contexts; Global Contexts). Hivyo hivyo, huwezi kufanikiwa endapo huwaelewi watumishi wa kada mbalimbali wa Mahakama. Jaji Mfawidhi hawezi kufanikiwa endapo hawaelewi wadau na watumiaji wa Mahakama,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Mbali na suala la udhibiti wa ucheleweshaji wa mashauri, Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha Waheshimiwa Majaji Wafawidhi kutosahau kutekeleza Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu 2022 inayosema ‘Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho Kuelekea Mahakama Mahakama Mtandao’.

“Mahakama ya Tanzania ilitoa ahadi muhimu sana kupitia Kaulimbiu yetu ya Wiki ya Sheria ya mwaka huu, hivyo ni muhimu tutambue kuwa baada ya mwaka mmoja tutaulizwa na kudaiwa ni nini tumefanya katika uwekezaji wa matumizi ya TEHAMA mahakamani. Wakati umefika sasa wa kutumia Mapinduzi ya Nne ya Viwanda na Akilibandia ‘Artificial Intelligence’ ili kufikia hatua ya kuwa na Mahakama Mtandao, nanyi ndio watekelezaji wakuu wa ahadi hiyo iliyotolewa mbele ya Mheshimiwa Rais na mbele ya Watanzania,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Madhumuni ya kikao kazi hicho cha siku mbili ni pamoja na kujenga ufahamu wa pamoja kuhusu hatua muhimu za kufuatwa hadi Mahakama-Mtandao, kujadili namna bora ya kukabiliana na wasiwasi, mitazamo na tamaduni hasi zilizojificha miongoni mwa watumishi dhidi ya matumizi ya teknolojia katika ufanisi na uwazi wa utoaji haki.


from MPEKUZI

Comments