NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikiliwa watu watano wakidaiwa kufanya mauaji ya kinyama ya watu watatu wa familia moja wilayani Ilemela, baada ya kuwataka kwa panga vichwani na shingoni.
Watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na vielelezo mbalimbali (vitu) zikiwemo mali za marehemu zilizoporwa ya baada ya tukio,likiwemo panga lililotumika kwa mauaji hayo.
Pia marehemu waliouawa kwenye tukio hilo walitambuliwa kuwa ni Mary Charles ambaye alikuwa mfanyabiashara wa mazao,binti yake,aliyetajwa kwa jina moja la Janet na mfanyakazi wao wa ndani, Monica Jonas, mwenyeji wa mkoani Kigoma.
Miili ya marehemu hao iliagwa juzi na kusafirishwa kwenda wilayani Sengerema kwa maziko,ambapo walizikwa jana kwenye makaburi ya Mission mjini Sengerema.
Tukio la mauaji hayo ya kinyama na ya kikatili,liliosabisha taharuki kwenye jamii, lilitokea Januari 18, mwaka huu,majira ya saa 5:30 huko maeneo ya Mto Jerry’s, mtaa wa Mecco Kusini,wilayani Ilemela.
Marehemu waliouawa kwenye tukio hilo na miili yao kutambuliwa,ni mfanyabiashara Mary Charles (42),Jenifa Fred au Nice (22) ambaye ni binti wa marehemu huyo na mfanyakazi wa ndani,Monica Jonas (19),wote wakazi wa Mecco Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusiana na mauaji hayo,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Ramadhan Ng’anzi,alisema linawashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji ya watu watatu wa familia kwa kuwakata kwa panga vichwani na shingoni.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa Januari 23,mwaka huu,kufuatia msako mkali na upelelezi wa kina uliohusisha vikosi vya upelelezi wa mauaji,makosa ya mtandao,intelejinsia na operesheni.
“Baada ya taarifa za tukio hilo kupokelewa,jeshi la polisi Mkoa wa Mwanza,lilianza upelelezi wa kina kuanzia Januari 19 hadi 23,2022 ambapo jumla ya watu watano walikamatwa wakiwa na vielelezo mbalimbali zikiwemo mali za marehemu zilizoporwa baada ya tukio na zimetambuliwa na ndugu wa marehemu,”alisema Ng’anzi.
Alisema ushirikiano uliotolewa na msiri mmoja kwa polisi uliwezesha kukamatwa kwa watuhumiwa hao ambao baada ya kuhojiwa walikiri kutenda kosa hilo la mauaji hayo ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa panga lililotumika kuua.
Ng’anzi alisema chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa kibiashara kati ya marehemu na baadhi ya watuhumiwa ambao walikuwa wakidaiana baada ya kukusanya na kupokea mzigo wa maharage kutoka Kigoma na kuupeleka kwa marehemu Mary.
Alieleza kuwa baada ya kubaini marehemu Mary hana uwezo wa kulipa fedha alizokuwa akidaiwa watuhumiwa walipanga na kufanya mauaji hayo.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Thomas Jilala Songay (26) msukuma mkokoteni na mkewe,Hajir Thomas (23),fundi cherehani, wote wakazi wa Utemini-Buhongwa na Douglas Vicent Malengwa (31), muuza duka la vifaa vya umeme,mkazi wa Buhongwa,wilayani Nyamagana.
Wengine ni Emmanuel Charles Lugaila (36), mwendesha mitambo katika mgodi wa Almasi Mwadui na mkazi wa Mwadui na Mecco Kusini na Emmanuel Matthew (19), mkazi wa Buhongwa katika Wilaya ya Nyamagana.
Mbali na watuhumiwa,silaha (panga) iliyotumika, jokofu moja aina ya Kyoto,luninga mbili ina ya Sum Sung inchi 18,redio mbili, jiko moja la gesi na godoro moja la ukubwa futi umeme, simu tatu aina ya Tecno za marehemu hao zilipatikana zikiwa zimefukiwa ardhini nyumbani kwa mmoja wa watuhumiwa.
Ilielezwa na Ng’anzi kuwa godoro hilo alinunuliwa marehemu Jenefa na mchumba wake na walitarajia kufunga naye ndoa ambapo ameacha mtoto mmoja wa mwezi mmoja huku marehemu Mary (mama yake) naye akiacha mtoto wa mwaka mmoja.
Aidha alisema askari waliohusika kuwakamata watuhumiwa hao halisi wa mauaji ya raia hao, walifanya kazi kubwa ya weledi bila kulala (usiku na mchana) na kufanikiwa kuwatia mbaroni siku chache baada ya tukio.
Kamanda huyo wa polisi alisifu ushirikiano wa wananchi kwa jeshi hilo na kuonya wenye tabia ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha vinginevyo sheria haitawacha, itawafuata popote wanapoihalifu.
Kwa mujibu wa Ng’anzi jeshi hilo linaendelea na upelelezi pamoja na kuwatafuta watuhumiwa wengine huku panga lililotumika kwenye mauaji hayo likipelekwa kwa Mkemia wa Serikali kwa uchunguzi wa kitaalamu wa ulinganifu wa vinasaba na alama za vidole.
“Upelelezi wa tukio hili unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwasaka baadhi ya watuhumiwa wengine ambao bado hawajakamatwa na mara baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria,”alisema.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment