Tanzania na Burundi zimeingia makubaliano ya awali ya utekelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Uvinza-Musongati hadi Gitega nchini Burundi.
Ujenzi wa reli hiyo utakapokamilika unatarajiwa kuimarisha huduma za uchukuzi kati ya Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano ya awali Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Tanzania, Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa reli hiyo ya kisasa unatarajiwa kuwa na urefu wa Kilomita 282 ambayo ni mwendelezo wa ujenzi wa reli ya SGR sehemu ya Tabora hadi Uvinza inayotarajiwa kupata Mkandarasi hivi karibuni.
Ujenzi huo umegawanywa katika sehemu mbili ambazo ni Uvinza hadi Malagarasi kwa upande wa Tanzania yenye urefu wa Kilomita 156 na Maragasi-Musongati hadi Gitega yenye urefu wa Kilomita 126.
Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa ujenzi wa reli hiyo utakuwa na manufaa kwa nchi za Tanzania na Burundi na utaibua fursa nyingi za ajira na biashara hivyo kukuza uchumi kwa wakazi wake.
“Usafiri wa reli ndio usafiri rahisi duniani hivyo reli hii itakayojengwa kwa ushirikiano itajengwa kwa viwango na uharaka kutokana na mahusiano mazuri ya nchi zetu mbili’, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesisitiza reli hiyo itakapokamilika itawezesha treni ya abiria kuwa na spidi ya kilomita 160 kwa saa na treni ya mizigo kuwa na spidi ya kilomita 120 kwa saa na itatumia umeme hivyo kuongeza chachu na uharaka na huduma za uchukuzi nchini.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa reli hii kunaongeza kasi ya mchakato wa utafutaji wa fedha na kusisitiza kuwa reli hiyo itajengwa kama ilivyopangwa.
Amesisistiza kuwa fedha za utekelezaji wa mradi huo zitapatikana na mradi utaanza kwa wakati kama Serikali ilivyojipanga na hivyo kuweka historia ya mataifa mawili kushirikiana kujenga reli na kukuza uchumi wa wananchi wake.
Waziri Dkt. Mwigulu amesema kuwa uwepo wa madini mengi kutoka Burundi kutawezesha reli hiyo kuwa na mzigo wa kutosha wa kusafirisha kwenda bandari ya Dar es Salaam na hatimaye kuongeza pato la Taifa.
Kwa upande wake Waziri wa Miundombinu wa Burundi, Dkt. Deo Nsanganiyumwani amesema kuwa ujenzi wa reli hiyo ni sehemu ya mikakati ya nchi hizo kukuza uchumi na kuimarisha ushirikiano baina ya wananchi wake.
Ujenzi wa Reli ya Uvinza-Musongati hadi Gitega ni muendelezo wa mikakati wa Serikali ya Tanzania kuhakikisha nchi hiyo inaunganishwa na nchi jirani ili kuwezesha mzigo mwingi unaopitia bandari ya Dar es salaam kwenda nchi jirani unatumia usafiri wa reli ambao licha ya kubeba mzigo mkubwa mara moja pia ni nafuu na wa haraka zaidi.
Imetolewa na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini Wizara Ya Ujenzi Na Uchukuzi
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment