Taarifa Kwa Umma Kutoka Jeshi La Polisi Mbeya Kuhusu Tukio La Mauaji


 Mnamo tarehe 31/01/2022 majira ya saa 04:30 alfajiri huko Mtaa wa Hasanga uliopo Kata ya Uyole Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya, mtu mmoja aitwaye JUSTIN NAMWINGA [55] Mwenyekiti wa Mtaa wa Hasanga alikutwa akiwa ameuawa kwa kuchomwa kisu kifuani chini ya titi la upande wa kushoto jirani na nyumbani kwake.

Awali kabla ya tukio hilo, JUSTIN NAMWINGA [55] alikuwa amelala na familia yake nyumbani kwake, walifika watu na kubisha hodi na kumjulisha kuwa kuna wezi nje, hivyo alitoka ili kutoa msaada baada ya muda kidogo majirani nao waliamka baada ya kusikia vishindo lakini walipofika nje walimkuta marehemu amelala kifudifudi huku akitokwa damu nyingi kifuani.

Chanzo cha tukio ni mapambano na wezi. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa uchunguzi wa kitabibu. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako mkali kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa wa tukio hili.

Aidha ninatoa rai kwa wananchi na yeyote mwenye taarifa za mtu/watu au kikundi cha watu waliohusika kwenye tukio hili watoe taarifa kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya ili watuhumiwa wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Imetolewa na:

[CHRISTINA A. MUSYANI – ACP]

KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.


from MPEKUZI

Comments