Prisca Ulomi na Paschal Dotto, Pwani
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa Serikali itatekeleza uwekaji wa mfumo wa anwani za makazi kwa muda wa miezi mitano badala ya miaka mitano kama ilivyokuwa itekelezwe hapo mwanzo kulingana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi Ibara ya 61(M) ya mwaka 2020 – 2025.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa semina ya utekelezaji mfumo huo katika Mkoa wa Pwani, Waziri Nape alisema kuwa zoezi hilo linafanyika kutokana na misingi mitatu ikiwemo ile ya Ilani ya CCM, Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 pamoja na Tanzania kuwa sehemu ya dunia kwani ni mwanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Umoja wa Posta Duniani (UPU).
“Msingi wa anwani za makazi unajengwa na msingi mitatu ikiwemo Ilani ya CCM ya 2020 – 2025, Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 pamoja na Tanzania kuwa mwanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) na Umojan wa Posta Duniani (UPU), suala hili linatekelezwa kwa miezi mitano tu badala ya miaka mitano kama Ilani inavyoelekeza, kwani itasaidia sana katika utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika Agosti mwaka huu”, amesema Waziri Nape.
Nape alisema kuwa katika utekelezaji wa zoezi hili hakuna mbadala isipokuwa ni kutekeleza kwa nguvu zote kwani Serikali ya Awamu ya Sita inadhamiria kuwasaidia wananchi katika kuboresha mawasiliano katika sehemu mbalimbali ikiwemo makazi yao, sehemu zao za biashara na maeneo mengine ya huduma za kijamii.
Aidha, Waziri Nape alisema utekelezaji wa zoezi la Anwani za Makazi ni jambo la kihistoria ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuacha alama kwa watanzania na lengo lake ni kurahisisha mawasiliano na kuifanya jamii kuwa ya kisasa zaidi bila kusahau kuimarisha ulinzi katika makazi yao.
Nape aliwataka viongozi wa Mkoa wa Pwani kusimamia kwa jitihada kubwa ili kurahisisha utekelezaji wa zoezi hilo kwani Mkoa huo bado uko nyuma katika utekelezaji huku akiwaomba uongozi wa CCM kutoka ngazi ya Mkoa mpaka ngazi ya tawi kuhamasisha jambo hilo kwani ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ambapo wenyewe ndiyo wasimamizi.
“Hapa hatuna kitu kingine zaidi ya utekelezaji wa zoezi hili, iwe mvua, iwe jua lazima jambo hili litekelezwe, Pwani mko nyuma sana mna kata 3 ambazo zimetekeleza jambo hili na nguzo 439 zimewekwa lakini bado kata 139, mahitaji yenu ni nguzo 75,392 na vibao 912,640 kwa hiyo utekelezaji wenu umefikia asilimia 1 bado asilimia 99”, amesema Waziri Nape.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa zoezi la uwekeji wa anwani za makazi litarahisisha utambuzi wa maeneo ya shughuli mbalimbali za mkoa wa Pwani yakiwemo maeneo ya viwanda.
“Anwani za Makazi na Postikodi ni mfumo mzuri ambao utatuonesha maeneo yetu mbalimbali kama mnavyofahamu kuwa Pwani ina viwanda vingi sana kwa hiyo uwepo wa anwani za makazi zitawarahisishia wananchi na zitarahisisha usafirishaji katika maeneo yetu”, alisema Kunenge.
Naye, Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza alisema kuwa Sekta ya Mawasiliano ni Sekta mtambuka ambayo inawezesha sekta nyingine kuendelea.
“Kama mnavyofahamu kwamba Sekta ya Mawasiliano ni sekta mtambuka, sekta zote zinategemea sekta hii, kwa hiyo uwekaji wa anwani za makazi itarahisisha mawasiliano kwa wananchi, Wizara ya Mawasiliano inashirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Ardhi ili kutekeleza jambo hili”, amesema Mhandisi Ichwekeleza.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment