Chande: Serikali Kuendelea Kujenga Uchumi Shindani Wa Viwanda

 


Na Benny Mwaipaja, WFM
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande, amewataka wadau wa Sekta ya Bima nchini kuhakikisha kuwa sekta hiyo inachangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu kwa asilimia tatu ifikapo mwaka 2030.

Mhe. Chande alitoa wito huo Mjini Zanzibar, wakati akifunga Kongamano la Tatu la Sekta ya Bima, lililowashirikisha wadau wa Sekta hiyo kutoka Bara la Afrika, katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Madinatul Bahri, Chukwani, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

“Mhakikishe kuwa idadi ya watu wanaofikiwa na huduma za bima nchini inaongezeka kutoka kiwango cha asilimia 15 kilichoripotiwa mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030 na hatimaye kuongeza mchango wa Sekta ya Bima kutoka asilimia 1 hadi kufikia asilimia 3 kufikia mwaka huo” alisema Mhe. Chande

Mhe. Chande alibainisha kuwa kuna changamoto ya ushiriki mdogo wa watanzania katika Sekta ya Bima ambapo takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kuwa kati ya kampuni 31 za Bima zilizosajiliwa nchini, wazawa walikuwa wanamiliki asilimia 100 kwenye kampuni 5 pekee.

Aidha, alihimiza umuhimu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu bidhaa za Bima ili kuwanusuru wananchi na majanga mbalimbali yakiwemo ya moto, ajali za barabarani, ulemavu wa kudumu na majanga mengine mengi akitolea mfano wa kuungua kwa masoko ya Kariakoo na Karume - Jijini Dar es Salaam, hivi karibuni.

“Majanga haya yanawarudisha nyuma wananchi kiuchumi na hata kuathiri familia zao kwa kukosa kinga stahili ya bima na kwamba kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii kunahitajika kuwepo kwa Sekta imara ya Bima inayoendana na ukuaji wa sekta mpya za kiuchumi na mabadiliko ya kiteknolojia” alisisitiza Mhe. Chande

Mhe. Chande, aliwataka wazingatie muundo wa uchumi wa Tanzania na kujielekeza zaidi katika kuondoa vihatarishi vinavyoathiri wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali wadogowadogo pamoja na kupanua mawanda ya huduma za bima ili kuongeza idadi ya watu wazima wanaopata huduma za Bima.

Mhe. Chande aliwataka wadau wote wa bima nchini kutekeleza Mpango Mkuu wa Miaka 10 wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/2021 hadi Mwaka 2029/2030, ulioainisha njia na mikakati mbalimbali ya kuimarisha Sekta ya Bima nchini.

Kwa uapnde wake Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware, alisema kuwa wadau wa Sekta ya Bima walioshiriki Kongamano hilo, pamoja na mambo mengine, wamekubaliana kuongeza uwekezaji katika teknolojia ili kupunguza uhalifu katika sekta hiyo.

Kongamano la Bima kwa Afrika la Mwaka 2022, lililokuwa na kaulimbiu ya kuongeza usambazaji wa huduma za bima na kukua kwa sekta ya Bima, limeshirikisha zaidi ya watu 300 kutoka nchi za Bara la Afrika.

Mwisho



from MPEKUZI

Comments