*Ampongeza Rais Samia kwa kutafuta fedha hizo kwa bidii
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameridhishwa na hatua iliyofikiwa kwenye ujenzi wa madarasa yanayotokana na fedha za maendeleo mkoani Lindi.
Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumanne, Desemba 28, 2021) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa huo kwenye uwanja wa ndege wa Nachingwea mara baada ya kupokea taarifa ya kila wilaya.
“Nimefurahi kusikia kuwa kuna maeneo kazi imekamilika kwa asilimia 100, wilaya nyingine zimefikisha asilimia 97, nyingine asilimia 75, na kikubwa zaidi ni kuweza kubakiza fedha baada ya kazi kukamilika,” amesema.
“Wilaya moja imebakiza shilingi milioni 35, nyingine shilingi milioni 33, na nyingine zaidi ya shilingi milioni 10. Hii ni dalili njema kwamba kazi hii ilisimamiwa vizuri, nawapongeza viongozi wote wa mkoa na wilaya, na pia wananchi waliojitokeza kuchangia nguvu kazi yao.”
Waziri Mkuu amemshukuru Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kutafuta fedha hizo ambazo zimekuwa mkombozi mkubwa kwenye kutatua changamoto mbalimbali katika huduma za kijami.
“Kwa fedha hii ambayo Mheshimiwa Rais ametumia jitihada kubwa kuzitafuta, na tumezipata tena kwa masharti nafuu, ni lazima tuzitumie ipasavyo. Nimefurahi sana kusikia nyie mmetumia vizuri fedha zenu kujenga madarasa na zimebaki.”
Waziri Mkuu amesema kutokana na mfano uliooneshwa na mkoa wa Lindi, anataraji kusikia mikoa mingine pia ikiwa imekamilisha kazi na fedha zimebakia hasa kwenye mikoa ambayo malighafi na vifaa ni rahisi ama haitoki mbali.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na viongozi wa Serikali na CCM wa mkoa na wilaya za mkoa huo, Mkuu wa Mkoa Lindi, Bibi Zainab Tellack alisema hatua za ujenzi uliobakia ni hatua za kumalizia kuweka madawati, nyingine kupakaa rangi na chache sana ni kuezeka.
Alisema licha ya kazi kubwa iliyofanyika, baadhi ya wilaya zimebakiza fedha lakini nyingi zimebakiza vifaa vya ujenzi kama nondo, saruji na rangi. “Tunataka tuombe kibali maalum cha kutumia hizi fedha zilizobaki na vifaa vilivyobakia ili kuboresha miundombinu kwenye maeneo mengine,” alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bw. Shaibu Ndemanga alisema alipokea sh. bilioni 2.26 ambapo kati ya hizo, sh. bilioni 1.1 zilikuwa ni za ujenzi wa madarasa 56 katika Manispaa ya Lindi na mengine 58 katika Halmashauri ya Mtama kwa thamani ya sh. bilioni 1.16.
“Katika Manispaa ya Lindi, tulikuwa na madarasa 35 ya shule za sekondari na madarasa 21 ya shule shikizi. Yote yameshakamilika kwa maana ya kuwekewa gypsum, marumaru na madirisha ya aluminium. Tumebakiza sh. milioni 35,” alisema.
Alisema katika Halmashauri ya Mtama madarasa 27 kati ya 58 yamekamilika kabisa na 31 yaliyobakia yako kwenye hatua tofauti. Alisema hapa hawajafikia hatua ya kubaini kiasi cha fedha kitakachobakia hadi wamalize kabisa kazi ya ujenzi na kuweka madawati madarasani.
Wilaya nyingine iliyofikisha asilimia 100 ya ujenzi ni ya Nachingwea. Wilaya hiyo ilipokea sh. bilioni 1.1 kwa ajili ya madarasa 69 ambapo madarasa 57 ni ya sekondari na 12 ni ya shule shikizi. Wilaya hiyo imebakiwa jumla ya sh. milioni 33.7.
Wilaya ya Liwale bado haijakamilisha sababu ya changamoto ya umbali lakini Mkuu wa wilaya hiyo ameahidi kuwa atakamilisha kabla ya Desemba 31, mwaka huu kama ilivyoelekezwa na Serikali.
Wilaya ya Kilwa ilipokea sh. bilioni 2.06 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 103 ambapo madarasa 28 yamekamilika kwa asilimia 100 na yaliyobakia yako kwenye asilimia 75 ya ujenzi wake.
Waziri Mkuu amewasili jimboni kwake Ruangwa kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment