Waziri Mchengerwa : Sitowasaliti Watumishi Wanaochapa Kazi Kwa Bidii, Weledi Na Uadilifu


Na. James K. Mwanamyoto-Kigoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema katika uongozi wake hatowasaliti katika kutetea stahiki zao Watumishi wa Umma wanaofanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu na uzalendo kwa taifa lao.

Akizungumza na Viongozi na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Mchengerwa amesema atahakikisha anasimamia haki na stahiki za Watumishi wa Umma nchini kwa lengo la kuwaongezea morali ya utendaji kazi kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia.

Kufuatia uamuzi wake wa kusimamia haki na stahiki za Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa ametoa rai kwa watumishi wote wa umma nchini kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuendana na kasi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan badala ya kufanya kazi kwa mazoea kwani wasipowajibika hatokuwa tayari kutetea stahiki zao.

“Pale ambapo tutabaini kuna mtumishi mzembe, mla rushwa na mbadhirifu wa mali za umma sitokuwa tayari kumtetea lakini nitakuwa tayari kupambana na kumtetea mtumishi yeyote mwadilifu, mchapakazi na mzalendo kwa taifa lake muda wote asubuhi, mchana, jioni na usiku,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Mhe. Mchengerwa amewaelekeza watendaji kufuatilia utendaji kazi wa watumishi walio chini yao mara kwa mara na kumtaka kila mtumishi kuongeza ubunifu katika eneo lake la kazi ili aweze kutoa huduma bora kwa wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na taasisi za umma nchini.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka waajiri kutenga bajeti ya mafunzo kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Watumishi wa Umma walio katika maeneo yao ili waweze kuwa na weledi, ubunifu na kuongeza ufanisi kiutendaji.

Waziri Mchengerwa yuko kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Kigoma yenye lengo la kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani humo.


from MPEKUZI

Comments