Bulyanhulu Yatenga Zaidi Ya Bilioni 3.7 Kuchangia Huduma Kwa Jamii Inayozunguka Mgodi Huo.

 


Na Mwandishi wetu..
Zaidi ya bilioni 3.7 zimetengwa na Kampuni ya uzalishaji madini ya dhahabu ya Bulyanhulu ambayo inaubia na Serikali kwa ajili ya uchangiaji huduma kwa jamii inayozunguka mgodi huo (CSR).

Hayo ameelezwa Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko alipotembelea mgodi wa Twiga Minerals Corporation Limited - Bulyanhulu unaomilkiwa kwa ubia kati ya Serikali kwa asilimia 16 na Barrick asilimia 84.

Aidha, taarifa za utafiti wa kijiolojia uliofanywa na Kampuni hiyo zimeonsha uwepo wa madini ya dhahabu katika eneo la kusini mashariki ambapo inapelekea kuongezeka kwa maisha ya mgodini kutoka 2036 hadi kufikia 2050.

Pia, imeelezwa kuwa, Twiga Minerals Corporation Limited inakamilisha miundombinu chini ya shimo ili mashine za uchimbaji ziweze kutumwa pasipokuwa na mtu yeyote kwenye mashine.

Aidha, Dkt. Biteko ameelezwa kuwa, kati ya asilimia 100 za Kampuni zinazo sambaza vipuri 36 ni kampuni za Kitanzania.

Awali, Dkt. Biteko alitembelea mgodi wa Ntambalale uliopo kijiji cha Wisolele kata ya Segese Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga ili kukagua shughuli za uchimbaji madini na kuzungumza na wananchi wadogo wa madini.

Dkt. Biteko amewataka wachimbaji wadogo wa Ntambalale kutembea kifua mbele na kutoruhusu mtu yoyote kuwaomba rushwa au kuwatishia na badala yake wafanye kazi kwa kujiamini.

"Tunataka Sekta ya Madini iendeshwe pasipokuwa na chembe chembe yoyote ya rushwa, akitokea mtu akawaomba hela, mwambieni aende akachimbe," amesema Dkt. Biteko.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Biteko amewataka wachimbaji wadogo wa Ntambalale kuchimba kwa kuzingatia usalama hususan katika kipindi hiki cha mvua za masika.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Msalala Iddy Kassim amemuomba Dkt. Biteko kusaidia kusogezewa umeme ili wachimbaji wadogo waweze kupunguza gharama za uzalishaji madini katika migodi wa Ntambalale.

"Naomba nichukue fursa hii kumuomba Mhe. Waziri utusaidie tutengenezewe miundombinu ya barabara pamoja na kusogezewa umeme ili wachimbaji wangu waweze kupunguza gharama za uendeshaji na uzalishaji wa madini katika mgodi huu," amesema Kassim.


from MPEKUZI

Comments