Askofu Josephat Mwingira kuhojiwa na Polisi


WAZIRI wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, George Simbachawene ameliagiza Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kumtafuta na kumhoji Askofu wa Kanisa la Efatha, Josephat Mwingira kuhusu tuhuma nzito  alizozitoa.

Ni baada ya Askofu Mwingira kutumia mahubiri ya jana Jumapili, tarehe 26 Desemba 2021 ya sikukuu ya Krismasi, katika Kanisa la Efatha Mwenge jijini humo, kutoa tuhuma mbalimbali ikiwemo ya kunusurika kwake kuuawa mara tatu

Simbachawene ameyasema hayo leo Jumatatu Desemba 27, 2021 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala mbalimbali.

Hatua hiyo ya Waziri Simbachawene imefuata baada ya kuwepo kwa taarifa mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii zikimnukuu Askofu Mwingira akutoa tuhuma mbalimbali ikiwemo kutishiwa maisha na mali zake kuteketezwa shambani kwake.

Askofu Mwingira amekaririwa akizungumza hayo kanisani kwake wakati wa ibada Jumapili Desemba 26, ambapo alieleza madhila aliyopitia wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya tano.

Akizungumzia suala hilo, Simbachawene amesema kiongozi huyo wa dini ametoa tuhuma nzito na kwamba inampa shida kwa sababu anajiuliza kwanini kiongozi huyo ameweza kukaa kimya kipindi hicho chote na kusubiri kuja kuzungumzia wakati wa Krismasi bila kutoa taarifa polisi.

"Kama itakuwa aliyoyasema ni kweli basi tutahitaji atusaidie kutupa taarifa zaidi. Kamanda wa polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam amtafute ili tuweze kupata maelezo yake...tumeona yaliyoandikwa mitandaoni, tungetamani tumsikie mwenyewe ili aingie kwenye rekodi za polisi," amesema waziri huyo.

Waziri Simbachawene ameongeza kwamba nchi hii inaongozwa kwa haki na sheria, hivyo mtu hawezi kukaa na hofu ya maisha yake lakini itaachwa hivi hivi.



from MPEKUZI

Comments