Abu Dhabi Yaahidi Kuendelea Kuipiga Jeki Tanzania Kimaendeleo


 Na Benny Mwaipaja, Abu Dhabi
SERIKALI ya nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu ya Abu Dhabi imeahidi kuendeleza ushirikiano katika masuala ya kiuchumi na kijamii na Serikali ya Tanzania ili kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Ahadi hiyo imetolewa mjini Abu Dhabi, Falme za Nchi za Kiarabu na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri anayeshughulikia masuala ya Rais, Sheikh Mansour bin Zayed Al Nanyan, baada ya kupokea ujumbe maalum kutoka kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliowasilishwa kwake na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Ikulu ya nchi hiyo.

Akizungumza baada ya mazungumzo yao ya faragha, Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa Sheikh Mansour ameahidi kutuma ujumbe maalum nchini Tanzania kwa ajili ya kuangalia miradi mbalimbali ya kimkakati inayotokelezwa hivi sasa na mingine mipya kwa ajili ya kutoa fedha.

Dkt. Nchemba aliitaja miradi iliyowasilishwa kwa Serikali ya Abu Dhabi kuwa ni ile ya uendelezaji wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi wa Ujenzi wa Bwala la Kuzalisha Nishati ya Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere, ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, kilimo na uvuvi pamoja na elimu.

“Kwenye sekta ya elimu tumejenga madarasa mengi, tumejenga vituo vya afya vingi sana na vingine viko vijijini lakini hatujajenga nyumba za watoa huduma wanaotakiwa kufanyakazi kwenye maeneo hayo” alisema Dkt. Nchemba.

Aidha, alisema kuwa wamejadiliana na Mhe. Sheikh Mansour bin Zayed Al Nanyan kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini zinazotokana na Tanzania kuwa lango la kibiashara kwa nchi zisizozungukwa na bahari ambazo zikitumiwa vizuri kama vile uwepo wa nishati ya mafuta na gesi, zitaifanya nchi ipae zaidi kiuchumi.

“Maeneo mengine tuliyojadiliana ni namna ya kuitumia na kuishirikisha sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa njia ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kuleta faida kwa pande zote mbili na wananchi kwa ujumla” aliongeza Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Jamal Kassim Ali, alisema kuwa mkutano wao na Naibu Waziri Mkuu wa Abu Dhabi uliangazia pia masuala ya Zanzibar ambapo miradi kadhaa ya kimkakati inayotaka ufadhili iliwasilishwa.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Manga Pwani kwa njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi, Ujenzi wa nyumba za makazi za gharama nafuu zipatazo 10,000 kwa ajili ya watumishi wa umma pamoja na wananchi wengine na uchimbaji wa mafuta na gesi.

“Zanzibar tuna fursa kubwa katika masuala ya uchumi wa blue ikiwemo uchimbaji wa mafuta na gesi, masuala ya uvuvi na utalii na wenzetu wamepiga hatua kubwa katika maeneo hayo, tukishirikiana nao katika maeneo hayo tutapiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii” alisema Mhe. Ali.

Aliishukuru Abu Dhabi kwa kuendeleza ushirikiano na Tanzania hususan Visiwa vya Unguja na Pemba ambapo nchi hiyo ya Kiarabu ilifadhili ujenzi wa Hospitali ya Wete-Pemba na kwa kuahidi kuwa tayari kuendeleza ushirikiano huo katika miradi mipya iliyowasilishwa kwao.


from MPEKUZI

Comments