Wizara Ya Afya Yapokea Dozi 125,520 Za Alu Zilizotelekezwa Bandarini


Na. WAMJW- DSM
SERIKALI imepokea dozi 125,520 za dawa ya kutibu ugonjwa wa Malaria aina ya ALU zenye thamani ya milioni 51.8 ambazo zimetolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya mfanyabiashara mwenye dawa hizo kutojitokeza kuchukua mzigo wake bandarini.

Akipokea kwa niaba ya Waziri wa Afya Dkt.Dorothy Gwajima,Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw.Daudi Msasi amesema dawa hizo wakizopokea zimeshafanyiwa uchunguzi na Mamlaka husika na zinafaa kwa matumizi ya binadamu

Ametaja dozi zilizopokelewa ni dozi za watu wazima ambazo ni tani tatu na kwamba zitaenda kugawiwa katika vituo vyote vya Afya nchini ili kuwasaidia wananchi katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria

“Tunawashukuru sana TRA kwa kuweza kuona umuhimu wa kusaidia jamii kama ambavyo wamekuwa wakifanya kuhakikisha kwamba tunakuwa katika nafasi moja pindi jamii inavyokumbwa na ugonjwa wa Maralia na sisi tutazifanyia mgao katika vituo vyote vya afya nchini na zitafanyiwa mgao na Bohariya dawa(MSD)”amesema Msasi

Ameongeza kuwa dawa hizo zitagawiwa na MSD kwa haraka ili wananchi waweze kunufaika kwa wakati kwani mwisho wa matumizi ni Novemba 2022.

“Dawa hizi zina nembo ya kijani wananchi watapatiwa kwa gharama ya nusu bei hata kwenye soko la kawaida tunashauri ukiona zina nembo ya kijani mteja anapatiwa kwa nusu bei”alifafanua

Naye,Meneja Msaidizi wa Shughuli za Bandari Bw.Aloni Kyando, alisema dawa hizo ziliiingia nchini Machi 6 mwaka 2020 na baada ya muda mteja hakujitokeza kufuata taratibu za kiforodha.

Pia Kyando ameongeza kuwa kasha la dawa hizo linajumla ya katoni 360 zenye jumla ya kilo 2170 na thamani yake ni zaidi ya milioni 51.8.



from MPEKUZI

Comments