Tanzania, Uswisi Kuimarisha Ushirikiano Zaidi


Na Mwandishi Wetu, Dar
Tanzania na Uswisi zimekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya, elimu na uchumi kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa pande zote mbili.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) alipokuwa katika maadhimisho ya miaka 40 ya Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi jana jioni jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula amesema kuwa katika miaka 40 ya Ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Uswisi, ushirikiano umeimarika na nchi hizi zimekuwa zikiufurahia kwa kipindi chote, na kuongeza kuwa “Uhusiano kati ya Tanzania na Uswisi ni mzuri na imara na umekuwa na manufaa kwa pande zote mbili,” amesema Balozi Mulamula

“Tunapozindua Mpango wa Ushirikiano kati ya Uswisi na Tanzania 2021-2024, ambao pamoja na mambo mengine, umejikita katika kuimarisha taasisi za serikali, kulinda na kuboresha afya na maisha ya vijana. Napongeza juhudi zinazofanywa na Uswisi katika maandalizi na ukamilishaji wa mpango wa maendeleo ambao sasa unatupeleka katika hatua nyingine ya utekelezaji,” ameongeza Balozi Mulamula.

Waziri Mulamula ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikichukua hatua madhubuti katika kupitia na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini ambapo Serikali na sekta binafsi wanafanya kazi kwa kutunga na kuboresha sera zitakazolinda na kuwezesha sekta binafsi kukua.

Pia Balozi Mulamula amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kurekebisha Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996. Utaratibu huu unafanywa kwa njia shirikishi ambayo inahusisha sekta ya umma na binafsi. Mipango hii itachangia katika kuweka mazingira mazuri zaidi ya uwekezaji na biashara kwa wawekezaji na biashara kutoka mataifa makubwa duniani na washirika wengine wa kibiashara.

Kwa upande wake, Balozi wa Uswisi nchini, Mhe. Didier Chassot amesema kuwa ushirikiano wa Uswisi na Tanzania umelenga zaidi uboreshaji wa barabara za vijijini, maendeleo ya kilimo, sekta ya afya na uwezeshaji wa asasi za kiraia. Aliongeza kusema kuwa, miradi ya maendeleo ya Uswisi nchini Tanzania imepanuka na kujumuisha shughuli mbalimbali katika nyanja za utawala, uvumbuzi, kuongeza ujuzi, mafunzo ya ufundi stadi na utamaduni.

“Ushirikiano wetu umekuwa na mafanikio mengi na katika kipindi cha miaka 40 iliyopita ambapo Uswisi imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa katika sekta za afya, ujenzi wa taasisi na mafunzo ya wafanyakazi wa afya,” amesema Balozi Chassot

Balozi Chassot ameongeza kuwa, Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kutoa msaada wa kuimarisha taasisi za serikali ili kuongeza mapato ya umma na kutoa huduma bora za umma, zenye usawa na zinazofaa zaidi kwa wananchi wote, kupunguza vikwazo vya kijamii na kiuchumi pamoja na kuimarisha matarajio ya kiuchumi kwa vijana.

Tunatazamia kuimarisha zaidi ushirikiano wetu na washirika wetu serikalini na mashirika ya kiraia katika kutekeleza agenda ya kimataifa ya kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya 2030.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Uswisi Bi. Patricia Dazi amesema kuwa wameridhishwa na hatua za maendeleo ambazo Tanzania imepiga na kuahidi kuendelea kushirikiana zaidi katika kuwainua wananchi kiuchumi.

“Uswisi imekuwa ikishirikiana na Tanzania kwa zaidi ya miaka 40 na tutaendelea kuudumisha ushirikiano huu kuwainua vijana kiuchumi ili kuwawezesha kufikia malengo yao kijamii na kisiasa,” amesema Bi. Dazi


from MPEKUZI

Comments