Serikali Yakaribisha Washirika Wa Maendeleo Kuchangia Sensa Ya Watu Na Makazi


Na. Saidina Msangi, WFM, Dar es Salaam
Serikali imetoa wito kwa washirika wa maendeleo kuiunga mkono katika kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwaka 2022.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya kimkakati wa ngazi za juu uliohusisha mawaziri, mabalozi, sekta binafsi na asasi za kiraia, jijini Dar es Salaam.

“Sensa ya Watu  na Makazi itaiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo, mageuzi ya sekta za kijamii na kuwezesha mamlaka za Serikali za mitaa kutekeleza mipango na kugawa rasilimali kulingana na mahitaji,”alisema Dkt. Nchemba.

Alishukuru washirika wa maendeleo kwa michango ambayo wameanza kutoa kufanikisha zoezi hilo muhimu kwa maendeleo na kuomba waendelee kuchangia zaidi kifedha na utaalamu  ili kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi  kufanyika kikamilifu.

Aidha, Dkt. Nchemba alisema kuwa mkutano huo utawezesha Serikali kushirikisha washirika wa maendeleo masuala ya kisera pamoja na mipango inayoendelea kutekelezwa ili kuwapa fursa ya kuangalia ushiriki wao katika utekelezaji wa mipango hiyo.

Alisema kuwa mkutano huo wa ngazi za juu umehusisha sekta binafsi na asasi za kiraia kwa kuwa ni wadau muhimu katika maendeleo na kuwa Serikali inaweka mazingira wezeshi ili ziweke kukua na kutengeneza ajira nchini, kukuza kipato cha wananchi na uchumi.

“Katika mkutano huu Serikali imejumuisha asasi za kiraia na sekta binafsi ili zipate  taarifa za maendeleo  na  kupata fursa ya kuona namna ya kushiriki katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya nchi”, alisema Dkt. Nchemba.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Wizara ya Fedha na Mipango  Zanzibar Mhe. Jamal Kassim Ali,  alisema kuwa  mkutanoo huo umetoa fursa ya nchi kukutana na washirika wa maendeleo na kuwasilisha mipango iliyopangwa ili waweze kuona namna ya kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mipango husika.

Aliiongeza kuwa mkutano huo umejumuisha sekta binafsi kutokana na kutambua  umuhimu wake  katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuwa mkutano huo utaleta tija kwa ustawi na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Washirika wa maendeleo Balozi wa Canada nchini Mhe. Pamela O’Donnell alisema kuwa washirika wa maendeleo kwa muda mrefu wamewekeza nchini mabilioni ya fedha kwa ajili ya kuchangia maendeleo endelevu ya nchi na kuwa wako tayari muda wote kuendelea kufanya hivyo katika masuala ya elimu, mazingira, afya na utawala bora na wanaamini kuwa fedha hizo watakazoendelea kuzitoa zitatumika kama ilivyokusudiwa.

Alipongeza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini kupitia sekta binafsi na kuwa hatua hiyo itachochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa ujumla na pia kwa kuzishirikisha asasi za kiraia katika mipango mbalimbali ya nchi.

Mhe. Pamela O’Donnell alisema kuwa washirika wa maendeleo wanapendekeza mambo manne kutiliwa mkazo ikiwemo usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi, demokrasia, utawala bora na haki za binadamu ambayo ni muhimu kwa amani na  maendeleo na jamii endelevu, kuweka mpango mzuri wa kupata nishati, kuhifadhi mazingira na uchumi wa bluu ambavyo visipofanyiwa kazi vina madhara katika maendeleo.

“Tunapongeza Serikali kwa uboreshaji wa mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji  na tunafurahi kuwa wawekezaji wengi wanaonesha nia ya kuja kuwekeza nchini lakini pia ni muhimu kuboresha zaidi kwa vitendo kwa kuwa wawekezaji wengi wanataka kuwepo na utawala bora, sera  na sheria zinazotabirika  ili kuwapa utulivu wa kuweza,”alisema Bi. O’Donnell.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Asasi za Kiraia Nchini Bi. Lilian Joseph alisema kuwa sasasi za kiraia nchini inapongeza hatua ya Serikali kuishirikisha katika maandalizi na utekelezaji wa   wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka mitano ambao  unatoa fursa kwa sekta binafsi na asasi za kiraia kushiriki katika mipango ya sera, kufuatilia na kufanya tathmini ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Ametoa wito kwa Serikali kuendelea kuwajengea mazingira wezeshi ya kufanikisha kutekeleza mipango na majukumu yao ya maendeleo kwa  ufanisi kwa kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakwamisha ikiwemo za kisheria, kodi na taratibu za  uendeshaji wa shughuli za asasi za kiraia.


from MPEKUZI

Comments