Rais Samia na Rais Museven wa Uganda washiriki kufunga Kongamano la Wafanyabiashara kati ya Tanzania na Uganda Ikulu jijini Dar


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, wameshiriki Kongamano la Wafanyabishara wa Tanzania na Uganda, lililofanyika jana tarehe 28 Novemba, 2021 katika viwanja vya Ikulu                Jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo lililojikita katika kuzungumzia fursa za biashara ya mafuta na gesi hususan maendeleo ya mradi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania.

Aidha, Mhe. Rais Samia amemshukuru Rais wa Uganda Mhe. Museveni kwa jitihada zake zilizowezesha kupatikana kwa mafanikio kuelekea utekelezaji wa mradi huo wa ushirikiano tangu alipofanya ziara ya mwisho Jijini Dar es Salaam tarehe 20 Mei, 2020.

Mhe. Rais amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda umezidi kuimarika hata katika kipindi hiki cha changamoto ya UVIKO 19 hivyo ni ishara nzuri katika kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye utekelezaji wa miradi ya ushirikiano.

Mhe. Rais Samia amesema kuwa Serikali ya Uganda imeiunga mkono Serikali ya Tanzania katika mambo muhimu ambayo yamesaidia katika maendeleo ya mradi wa Bomba la kusafirisha mafuta. Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa wataalamu wa Tanzania na Uganda kuangalia masuala muhimu yatakayowezesha kuleta ushirikiano katika sekta ya mradi huo.

Kwa upande mwingine, Mhe. Rais Samia amewataka wadau kutoka Sekta binafsi kutumia fursa zinazopatikana kutokana na utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa Serikali za nchi hizo mbili zinafanya jitihada kuhakikisha Sekta hiyo na jamii za nchi zote mbili zinanufaika na mradi huo.

Mhe.Rais Samia amewaeleza wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Uganda kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Taasisi yake ya Utafiti na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO) ina uwezo wa kutoa huduma za kibobezi ikiwemo kufanya ukaguzi katika mabomba ya kuhifadhi na kusafisha mafuta na gesi.

Mhe. Rais Samia amehimiza nchi zote mbili kuendelea kuvutia uwekezaji katika nyanja mbalimbali ikiwemo viwanda vinavyotumia malighafi za ndani hususan katika sekta za kilimo na maliasili. Hivyo, Mhe. Rais Samia ametoa wito kwa wawekezaji wa Tanzania kuwekeza Uganda na Uganda kuwekeza nchini Tanzania.

Kwa upande wa Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni pamoja na mambo mengine,  amesema kuwa mradi wa Bomba la Mafuta ghafi utakuwa na manufaa kwa pande zote mbili  na kusaidia kutoa  ajira kwa wananchi wa nchi hizo.

  

Jaffar Haniu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.



from MPEKUZI

Comments